Juma Abdul avunja ukimya

Muktasari:

Abdul  ni mmoja wa beki wa kulia anayesifiwa kwa kumudu kupiga krosi kali zinaozaa mabao kwenye kikosi cha Yanga  lakini siku hizi amekuwa hapati nafasi mara kwa mara kwenye kikosi  hicho jamabo ambalo limekuwa likiwakwaza mashabiki wa klabu hiyo.

NAHODHA Msaidizi wa Yanga, Juma Abdul ambaye kwa mara ya kwanza juzi Alhamisi alianza kikosi cha kwanza msimu huu na kucheza kwa dakika 90, amevunja ukimya na kuwatuliza mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.
Abdul ameweataka mashabiki hao wa Yanga watulie kwani muda si mrefu timu hiyo itakuwa tishio na hata ubingwa inaweza kuchukua iliyoupoteza misimu miwili iliyopita mbele ya watani wao, Simba.
Matokeo ya sare ya 3-3 iliyoyapata Yanga juzi dhidi ya Polisi Tanzania yaliamsha hasira za mashabiki waliofika Uwanja wa Uhuru kushuhudia mchezo huo wakirushia maneno viongozi na baadhi wakimtaka Kocha Mwinyi Zahera asepe zake.
Zahera alikuwa jukwaani  katika mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya  kufungiwa mechi tatu na Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi lakini haikuwazuia mashabiki kumtolea maneno makali baada ya mchezo huo kwa madai timu haichezi vizuri.
Hata hivyo, Abdul aliyechangia mabao mawili kwa kutoa pasi zilizotupiwa nyavuni na Mrisho Ngassa na David Molinga, alisema mashabiki hawatakiwi kuwa na hasira na kukata tamaa bali kuwa na umoja na kuiunga mkono timu yao ili ifanye vizuri zaidi.
"Mashabiki wasikate tamaa kwani ligi bado mbichi ndio kwanza mechi ya pili  tu  na kuna  mechi nyingi zinakuja  ambazo naamini tutafanya vizuri na hata ubingwa tunaweza kuchukua," alisema na kuongeza;
"Kocha ndio kwanza anatengeneza timu kwani wachezaji wengi wapya, ndio maana unaona bado hana kikosi cha kwanza. Muhimu wote tushirikiane kuanzia wachezaji, viongozi na mashabiki na tuwe na umoja naamini kabisa huko mbele tutafanya vizuri."
Abdul  amekuwa hapati nafasi ya  kucheza kwa muda mrefu lakini juzi alianzishwa kikosi cha kwanza na kufanya vizuri huku akitoa pasi ya bao la kwanza la Yanga lililofungwa na Mrisho Ngassa.
"Nafurahi  nimeanza mchezo dhidi  Polisi Tanzania baada ya kipindi kirefu kuwa nje ya uwanjan kutokana na majeruhi kwani hata nilivyopona, kocha alinipa muda nifanye mazoezi niwe fiti "alisema Juma Abdul.