KMC FC waamua kugoma mapema

Friday February 21 2020

 

By SADDAM SADICK, MWANZA

STRAIKA wa KMC, Hassan Kapalata amesema licha ya timu yao kuwa kwenye wakati mgumu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, bado anaamini watapambana na kuepuka kushuka daraja na wataanza mipango yao mbele ya Ndanda.
KMC licha ya kuwa na kikosi kizuri mpaka sasa kimeshindwa kwenda na kasi ya msimu uliopita, walioshiriki ligi kwa mara ya kwanza na kumaliza msimu wakiwa wa nne na kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Mpaka sasa timu hiyo ina pointi 22 baada ya kushuka uwanjani mara 23 na kesho Jumamosi watakuwa Mtwara kuvaana na Ndanda ambao wamekuwa na matokeo mazuri kwa siku za karibuni, kwani imechezesha mechi sita na kushinda nne na kutoka sare mbili ikiwamo ya juzi dhidi ya Azam.
Kapalata alisema licha ya hali ngumu waliyonayo ya matokeo, lakini wameapa kutoshuka daraja kwa vile timu yao ina wapambanaji na nyota wenye vopaji vya soka na wataanza kazi kwa Ndanda wakitaka kutibua rekodi ya Kocha Meja Abdul Mingange ambaye hajafungwa tangu apewe timu.
"Hatuwezi kushuka Daraja licha ya matokeo haya, kimsingi tumeshakaa na kujadili mwenendo na tumeazimia la kufanya na matarajio yetu ni kufufukia kwa Ndanda," alisema Kapalata.
Nyota huyo wa zamani wa Mwadui FC, aliongeza Ligi imekuwa ngumu haswa ishu ya timu nne kushuka Daraja imewashtua wengi jambo linalowafanya KMC kuumiza kichwa kujinasua nafasi za chini na kudai hataki kurudi Daraja la Kwanza ndio maana wamekula kiapo kupambana kujinusuru.
"Ni kweli Ligi ni ngumu na ina ushindani mkali na hili ni kutokana na mabadiliko ya kikanuni kwa timu nne kushuka Daraja moja kwa moja, KMC hatutaki hata kucheza Play Off, tutapambana kufanya vizuri hata kwenye FA" alisisitiza.

Advertisement