Kagera Sugar yaichapa tatu bila Yanga ya Mbelgiji Eymael

Dar es Salaam. Kagera Sugar imemkaribisha kocha mpya wa Yanga Mbelgiji Luc Eymael kwa kipigo cha mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kocha Eymael katika mchezo wake wa kwanza tangu achukue jukumu hilo alitumia muda mwingi kugombana na mwamuzi wakati timu yake ikipokea kipigo hicho kutoka kwa Kagera Sugar iliyokuwa ikicheza kwa nidhamu ya hali ya juu ya mchezo.

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yusuf Mhilu alifunga bao la kwanza katika dakika 13, kabla ya Ally Ramadhani (68) na Peter Mwalianzi (89) kuhitimisha kalamu hiyo ya Kagera Sugar dhidi ya wachezaji kumi wa Yanga.

Kagera Sugar iliyokuwa imepoteza michezo mitano iliyopita ilianza mchezo huo vizuri bila ya kuwa na hofu na mpira wa pasi nyingi walinzoingia nazo Yanga.

Uzembe wa beki wa Yanga, Kelvin Yondani kushindwa kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Mhilu ambao ulimkuta mfungaji huyo aliyepiga shuti kali na kujaa wavuni katika dakika 13.

Akiwa pembeni kushoto ya mabeki wa Yanga, Lamine Moro, Kelvin Yondani na Paul Godfrey, kiungo Yusuph Mhilu aliachia shuti lililomshinda kipa Farouk Shikhalo na kujaa wavuni baada ya beki ya Yanga kujichanganya.

Licha ya Yanga kupambana kusawazisha kupitia kwa Haruna Niyonzima, Patrick Sibomana, Mapinduzi Balama na Ditram Nchimbi, lakini walikutana na kigingi kutoka kwa mabeki wa Kagera walioongozwa na nahodha Juma Nyoso.

Yanga ilijikuta ikicheza pungufu baada ya Banka kupewa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea faulo Kelvin Sabato wa Kagera dakika ya 44.

Mchezaji huyo akiwa anatoka nje kocha Eymael alimuita na kumkumbatia.

Yanga ilipata pigo katika dakika 37, baada ya kiungo wake Mohammed Issa ‘Banka’ kupewa kadi nyekundu ikiwa ni njano ya pili na kufanya Kagera Sugar kwenda mapumziki wakiwa mbele kwa bao 1-0.

Mbali na kipigo hicho, kocha wake mpya Eymael alijikuta akiingia uwanjani kumfuata mwamuzi, Abdallah Mwinyimkuu na kuonekana kuzoza mara baada ya filimbi ya mapumziko.

Tukio hilo lilifanya kocha huyo kuibua maswali kwa mashabiki waliojitokeza kwa uwanjani hapo.

Eymael ambaye anaiongoza Yanga kwa mara ya kwanza alionekana muda wote akitoa maelekezo kwa wachezaji wake na mara kadhaa alionekana kumlalamikia mwamuzi wa mezani wakati mechi ikiendelea.

Kipindi cha pili Kagera Sugar ilikuwa bora na kutumia vizuri upungufu wa mchezaji wa Yanga kulishambulia lango la wapinzani wao walionekana kukosa mipango  bora.

Kagera ilipata bao la pili dakika 68 kupitia kwa Ally Ramadhan aliyeingia akitokea benchi baada ya makosa ya Niyonzima ambaye alijichanganya na kunyang'anywa mpira akiwa nje kidogo ya eneo la 18.

Baada ya kunyang'anywa mpira, Niyonzima alijaribu kukaba lakini alichelewa kabla ya Kagera kugongeana kwa haraka na kumkuta Ramadhan aliyeachia shuti lililomgonga Moro na kujaa wavuni.

Nahodha wa Yanga, Niyonzima amelazimika kuomba radhi kwa wenzake baada kutokana na kusababisha bao hilo.

Baada ya bao hilo Yanga ilipotea kabisa mchezo na kuwaacha Kagera Sugar kucheza wapendevyoa.

Kagera Sugar ilihitimisha kwa kufunga bao la tatu katika dakika 86, David Luhende alipiga krosi iliyomkuta Mwalianzi alipiga kichwa na kujaza mpira wavuni.

Kocha wa Kagera, Mecky Mexime alisema ushindi huo ni mipango yao kwani hana kawaida ya kupaki basi.

"Sina kawaida ya kupaki basi, mbinu zetu ndizo zimetupa ushindi, uwa tunacheza kwa mbinu tu kama mpinzani wetu hajaelewa tunamfunga na ndicho kimetokea kwa Yanga," alisema Maxime.