Kagera Sugar yatibua mipango ya Simba SC

Muktasari:

  • Simba ilitengeneza rekodi kwenye Ligi Kuu kwani tangu Novemba 23 mwaka jana ilipotoka suluhu na Lipuli na ilikuwa ikishinda tu mechi zake hadi jana ilipolala dhidi ya Kagera Sugar.

Kagera. Historia imejirudia kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Kagera baada ya Kagera Sugar kuichapa Simba mabao 2-1 na kutibua rekodi ya mabingwa hao watetezi ya kutopoteza mechi za ligi kati ya michezo 11 mfululizo iliyopita.

Simba yenye bahati mbaya na Kanda ya Ziwa, huo ni mchezo wake wa pili kupoteza baada ya kufungwa bao 1-0 na Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, mchezo wa kwanza.

Hata hivyo, matokeo hayo bado yanaibakisha Simba kwenye nafasi yake ya tatu ikiwa na pointi 60 ikiwa nyuma ya Azam yenye pointi 66 wakati Yanga ina pointi 64.

Simba ilitengeneza rekodi kwenye Ligi Kuu kwani tangu Novemba 23 mwaka jana ilipotoka suluhu na Lipuli na ilikuwa ikishinda tu mechi zake hadi jana ilipolala dhidi ya Kagera Sugar.

Ukiacha hayo, mabao mawili yaliyofungwa na Kassim Hamis na Ramadhan Kapera yalitosha kuipa ushindi Kagera na kuitibulia Simba iliyo katika harakati zake za kusaka ubingwa wa ligi.

Aprili 4 Mwaka 2017 Simba ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera kwenye Uwanja wa huo, na kuwatibulia Wekundu hao wa Msimbazi katika mbio zao za ubingwa kuwaacha watani zao Yanga wakichukua kilaini.

Hamis aliipatia Kagera Sugar bao la kuongoza dakika ya 17 akimalizia kazi nzuri ya Venance Ludovic kutokana na mabeki wa Simba kushindwa kumzuia vyema.kuingia kwa bao hilo kulizidi kuwachanganya Simba na kujikuta wakipoteana huku Kagera Sugar wakicheza soka la kiwango na kufunga bao la pili dakika ya 42 kupitia kwa Ramadhan Kapera aliyefunga kwa kichwa.

Simba watajilaumu wenyewe kwa kucheza chini ya kiwango na kuwapa nafasi wapinzani kutawala mpira kipindi chote cha kwanza hivyo kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili Simba walifanya mabadiliko kwa kuwatoa James Kotei na Haruna Niyonzima na kuwaingiza Hassan Dilunga na John Bocco mabadiliko yaliyoinufahisha Simba na kupata bao la kufutia machozi.

Bao hilo la Simba lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 62 baada ya wachezaji wa Simba kugongeana pasi murua.

Baada ya bao hilo, Simba walirejea mchezoni na kulishambulia lango la Kagera Sugar kama nyuki lakini kutokana na kukosa utulivu eneo la hatari, walishindwa kusawazisha.

Pia uchoyo wa wachezaji hao wa Simba uliwagharimu dakika ya 79 baada ya Chama kuambaa na mpira na kama angefanya uamuzi wa kuwapa wenzake pasi; Okwi na Kagere pasi waliokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga lakini akapoteza.

Simba itateremka tena dimbani Jumanne kuikabili Alliance FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime aliwapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo yake na kupata ushindi dhidi ya Simba.

“Kabla ya mchezo niliwaambia wachezaji wangu kuwa unapocheza na timu kubwa zenye wachezaji wengi wanaoamua matokeo inabidi kumaliza mchezo mapema na ndicho tulichofanya.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema hawakuanza vizuri mchezo huo na kuja kuzinduka mwishoni wakati muda umeshaenda hivyo wanasahau mechi hiyo na kujipanga kushinda kwa ajili ya mechi ijayo.

Katika mechi nne ambazo Simba imecheza kwenye Uwanja wa Kaitaba tangu 2015 imeshinda tatu na kupoteza mbili wakati kwenye Uwanja wa Taifa, imeshinda mechi tatu na kupoteza moja.