Kiingilio nusu fainali Cecafa buku tu

Muktasari:

  • Fainali ya mashindano ya Cecafa kwa wanawake itachezwa Jumatatu ijayo kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini.

BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), limetangaza bei ya kiingilio kwa michezo ya nusu fainali ya mashindano ya wanawake ya Afrika Mashariki kuanzia kesho Jumamosi ambacho kitakuwa ni Sh 1000.
Mwenyekiti wa kamati ya ndani ya mashindano hayo, Oscar Milambo alisema lengo la kuweka kiingilio hicho ni kudhibiti namba ya mashabiki.
"Mashindano ya mwaka huu unaweza kuona ni ya aina yake na yanaonyesha kwamba kwa upande wa soka la wanawake hapa Afrika na Mashariki kuna jambo limefanyika.
"Kuanzia mechi za hatua ya nusu fainali tumeweka kiingilio ambacho kitakuwa ni Sh 1000 kwa mashabiki na lengo la kufanya hivyo ni kujaribu kudhibiti idadi ya mashabiki lakini bado tunasisitiza kwamba namba ikitosha hatutaruhusu shabiki yeyote kuingia hata kama atakuwa na fedha," alisema Milambo.
Mechi ya kwanza ya nusu fainali itakuwa ni baina ya Kenya watakaovaana na Burundi kuanzia saa 7.45 mchana wakati wenyeji Kilimanjaro Queens watakutana na Uganda katika mechi ya pili ya hatua hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 jioni.
Ofisa Habari wa mashindano hayo, Gift Macha alisema mechi za hatua hiyo ya nusu fainali hazitokuwa na dakika za nyongeza pindi dakika 90 zitakapomalizika matokeo yakiwa sare na badala yake mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penati