Kisa Yanga: Simba yaomba kuahirishiwa mechi Dar

Muktasari:

  • Umekuwa ni utaratibu kabla ya mechi ya watani wa jadi kujiandaa kwa wiki mmoja

Mwanza. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba imetuma maombi ya kusogezwa mbele mechi yao dhidi ya Biashara United iliyopangwa kuchezwa wiki ijayo Septemba 27, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Simba ambao wamepokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbao jana imetuma maombi hayo ni kutokana na mechi hizo kupangwa tarehe za karibu na mechi yao na Yanga ikiwa ni siku mbili tu.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' alisema hawataweza kucheza mechi hiyo kwani kikosi chao kitakuwa hakijafanya maandalizi ya kutosha baada ya mechi za mikoani.

"Tumeomba mechi ya Biashara isogezwe ili angalau wapate muda wa kujiandaa na mechi yetu na Yanga maana ukiangalia ratiba inatubana sana hatujapumzika.

"Tumecheza mechi mfululizo za mikoani muda wa kujiandaa hautoshi na hiyo ni moja ya mechi ngumu kama inavyofahamika hivyo mechi ya katikati ya wiki haitakuwepo," alisema Try Again

Simba inacheza mechi tatu za mikoani ambapo walianza na Ndanda na sasa wapo Kanda ya Ziwa ambako wana mechi mbili.

Tayari Simba wamecheza na Mbao ambapo wamepoteza na keshokutwa Jumapili wanacheza na Mwadui uwanja wa CCM Kambarage.

TFF itapaswa pia kusogeza mbele mechi ya Yanga dhidi ya JKT Tanzania inayotarajiwa kuchezwa Septemba 26 ili nao wajiandae na mechi hiyo ya watani.