Kisa namba! Manula, Kakolanya wazua jambo Simba SC

Muktasari:

Tangu baada ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, kipa Manula amepoteza namba yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao watetezi.

Dar es Salaam.Ushindani wa namba wa makipa wa Simba, Aishi Manula na Beno Kakolanya uanza kuibui minong’ono kuhusu nani anayestahili kuanza katika kikosi cha kwanza.

Tangu baada ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga, kipa Manula amepoteza namba yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao watetezi.

Kukaa nje kwa Manula kumewaibua wadau wa soka nchini na kuwataka mashabiki wa Simba wawe watulivu na kuacha kumbeza kipa huyo kwani amecheza kwa kiwango kikubwa akiwa na timu hiyo.

Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka nchini, Kenny Mwaisabula alisema Manula amekuwa na kiwango kizuri kwa mechi zote alizocheza lakini anashangazwa kuona kipa huyo akibezwa kipindi hiki.

Mwaisabula alisema kipa huyo anatakiwa kupewa heshima kwani hata mechi za msimu huu alizocheza hajafanya vibaya, huku akisifu kiwango cha Beno Kakolanya akiamini ushindani unazidi kuwa mkubwa.

"Wanaweza wakacheza pamoja na wote wakawa vizuri halafu wakaitwa timu ya Taifa, Mwameja na Steven Nemes waliwahi kuwa Simba pamoja na baadae wakaenda kucheza timu ya Taifa, walikuwa viwango," alisema.

Aliongeza kwa kusema hata Nemes alipoenda Yanga alikutana na Riffat Said na bado walicheza kwa viwango, kikubwa ifanyike mabadiliko kwasababu Manula na Kakolanya wote ni makipa wazuri.

Katibu mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah alisema Manula ni kipa mzuri, lakini anajua aliondolewa katika kikosi cha Simba baada ya mchezo wao dhidi ya watani wa jadi.

"Makosa yale wameyalundika wenyewe na kuwa mengi, kwahiyo wameyawasilisha kwa pamoja, lakini Manula ni kipa mzoefu ambaye anatakiwa kuaminiwa zaidi," alisema.

Aliongeza kwa kusema kocha ndio mwenye uamuzi wa mwisho nani acheze, lakini kama kaingiliwa majukumu basi ni tatizo.

Licha ya kupewa majukumu akiwa na presha ya kuhakikisha anaendelea kukaa golini kwa kutopoteza mchezo wowote, Kakolanya amecheza mechi mbili za Ligi Kuu huku zote wakishinda. Pamoja na mechi ya Kombe la Azam Federation amecheza mechi moja nayo wakiibuka na ushindi.