Kocha Serengeti Boys bado ana hesabu za kupenya Afcon

Dar es Salaam. Hakuna kukata tamaa! Ndio kauli iliyotolewa na kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kuelekea mchezo wa mwisho wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U17) dhidi ya Angola kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 10:00 jioni.

Matumaini ya Serengeti Boys kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo ni finyu lakini kimahesabu bado nafasi ipo ikiwa mambo mawili yatatokea kwa wakati mmoja leo.

Kwanza ni Serengeti Boys yenyewe kushinda mchezo wake dhidi ya Angola kwa mabao kuanzia 4-0 ili ifikishe pointi tatu kwenye kundi A na kuwa na utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ambao ni 0.

Jambo la pili linalopaswa kutokea pindi Serengeti Boys ikiibuka na ushindi ni Uganda kupoteza dhidi ya Nigeria kwa kichapo cha kuanzia mabao 3-0, jambo litakaloifanya utofauti wa mabao yake ya kufunga na kufungwa uwe hasi moja (-1)

Kwa vile baada ya matokeo hayo timu tatu zitakuwa zimelingana pointi kwenye Kundi A, Serengeti Boys itapenya na kuziacha kwenye mataa Angola na Uganda ikiungana na Nigeria kwenda nusu fainali.

Mahesabu hayo yameonekana kuipa morali Serengeti Boys ambayo kupitia kwa kocha wake mkuu, Oscar Mirambo na nahodha Mourice Abraham wametamba kupambana hadi tone la mwisho la damu kuhakikisha wanapenya.

“Tunaamini kwenye nafasi ambayo ipo. Timu ya taifa ilifuzu vipi kwenda Fainali za Mataifa ya Afrika. Ilipenya kwa kutegemea pia matokeo ya mechi nyingine na lengo likatimia. Huu ni mchezo wa mpira lolote linaweza kutokea.

Tuna mechi moja ya kucheza. Jambo zuri kwenye hii mechi ya mwisho ni kuwa bado tuna nafasi ya kupita ikiwa tutapata ushindi, na Uganda atapoteza. Tunataka kusaka ushindi kesho halafu baada ya hapo tutaangalia mechi ya Uganda ikoje,” alisema Mirambo.

Kwa upande wake nahodha Abraham alisema kuwa wachezaji wanepokea matokeo ya mechi mbili zilizopita dhidi ya Nigeria na Uganda kama changamoto ya kuwafanya wapambane zaidi.

“Kuna wakati kile unachokitegemea unaweza usikipate hivyo sisi ni kama tulijikwaa hivyo tunapaswa kuinuka na kusonga mbele,” alisema.