Breaking News

Kocha kiziwi apania kufundisha klabu kubwa

Tuesday December 3 2019

 

By AFP

Ben Lampert si kocha wa kawaida kama wengine. Badala ya kupiga kelele kutokea benchi, kocha huyo kiziwi hutoa maelekezo yake kwa lugha ya alama.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 34 na ambaye anaifundisha Brentford FC Community Sports Trust, anathibitisha kuwa ni kioo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia na watoto wasio na tatizo hilo na ametajwa kuwania moja ya vipengele katika Tuzo za Makocha wa Uingereza zitakazofanyika keshokutwa Alhamisi.
Lampert, ambaye alikuwa mchezaji katika kikosi cha Uingereza kilichotwaa ubingwa wa Olimpiki kwa Viziwa mwaka 2005 nchini Australia, anataka awe kocha wa klabu ya kulipwa hapo baadaye.
"Ndoto yangu ni kufundisha soka katika kiwango cha juu, ama iwe shule za soka au klabu," aliiambia AFP kabla ya kuanza mazoezi na timu ya wachezaji wavulana wenye umri chini ya miaka 10.
"Ili tu kuwa aina ya watu ambao wanaamini kuwa vikwazo hivi vinaweza kuvunjwa na kuondolewa. Suala la umri halitakuwa na maana.
"Sijui ni mpaka umri wa miaka 18 au zaidi. Ni suala la kufikia mafanikio na kuwa mfano ambao watu wenye uziwi wanaweza kuangalia na kusema 'Ben ameweza, kwanini nishindwe?'"
Lampert, baba wa watoto wawili, alisema kuna mtazamo kwamba ni vigumu kwa watu wenye ulemavu wa kusiki kufikisha ujumbe kwa wengine lakini anadhani si sahihi.
"Wanadhani haiwezekani kwangu kufanya hivi au mtu mwingine yeyote kiziwi kufanya hivyo," alisema, akizungumza kwa kumtumia mkalimani ambaye alimsaidia katika kazi magharibi mwa London.
"Unajua, wanadhani si kitu kinachoweza kutokea, lakini inawezekana. Wakati ninapopata nafasi ya kuzungumza na watu hawa, wanabaini hilo.
"Ni suala la mawasiliano tu. Mwisho wa siku, kuna njia nyingine za mawasiliano, si kitu cha mwelekeo mmoja."
Lampert, ambaye alishiriki katika kukimbiza mwenge wa Olimpiki mwaka 2012, alisemas kuwasiliana kwa kutumia lugha za alama ni changamoto inayofanana na wanayokutana nayo makocha ambao Kiingereza si lugha yao ya kwanza.
"Wana stadi au mahitaji yanayotakiwa kuwa makocha wakubwa. Ni kikwazo cha lugha," alisema Lampert, ambaye ametajwa kuwania tuzo ya Changing Lives (kubadili maisha).
"Unajua, hiyo ndiyo njia pekee ya kuwa katika njia sahihi. Hakuna tofauti, kwa maoni yangu, kwa mtu kiziwa kwa maana hiyo."
Lampert, ambaye pia ni kocha wa timu ya taifa ya England ya soka, alisema kuwa kiziwi si kizuizi cha jinsi anavyoangalia mchezo, akieleza kuwa soka ni mchezo wa kutazamwa.
"Kama mtu mwenye tatizo la kusikia, ni sahihi kabisa kwangu na kufikiria kuhusu nafasi za watu uwanjani na mbinu na wapi kwa kupeleka wachezaji."

Advertisement