Lamine amtaka Yondani Yanga

Dar es Salaam. Lamine Moro amesema Kelvin Yondani ni beki mwenye kiwango bora katika kikosi cha Yanga.
Akizungumza jana, Lamine alisema anakuwa na amani akicheza na Yondani kulinganisha na Ally Sonso au Said Juma ‘Makapu’ ingawa wote ni mabeki hodari.
Lamine alisema amezoea kucheza na Yondani kwa kuwa ni beki bora na amekuwa akitumia uzoefu wake kuokoa hatari tofauti na Sonso au Makapu. Alisema Yondani ni beki anayezungumza muda wote uwanjani na wamekuwa na mawasiliano ya karibu katika uchezaji kulinganisha na Sonso aliyedai si mzungumzaji.
“Nina mawasiliano mazuri na Yondani, tunazungumza uwanjani namna ya kucheza na kukabiliana na maadui wetu. Sonso haongei na Makapu bado ni mgeni katika eneo la ulinzi,” alisema Lamine.
Mchezaji huyo raia wa Ghana, alisema pamoja na kasoro hizo Sonso na Makapu ni mabeki wanaojituma na watakuwa imara wakiendelea kupangwa katika mechi za Yanga.
“Makapu ni beki mzuri ndio kwanza kacheza mechi nne na amefanya vizuri anatengenezwa kucheza kwasababu nimeambiwa alikuwa kiungo mkabaji kucheza kati akiendelea kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara atamrithi Yondani namshauri apambane zaidi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ana furaha kucheza na beki yeyote atakayepangwa naye katika safu ya ulinzi kwa kuwa kazi yake ni kucheza mpira na si kuchagua mchezaji wa kucheza naye.
Tangu Kocha Mbelgiji Luc Eymael alipotua Yanga kujaza nafasi ya Mwinyi Zahera, amekuwa akimtumia Lamine kucheza na Sonso au Makapu.
Kocha huyo aliwahi kukaririwa na gazeti hili akisema Yondani alichelewa kuripoti kambini kwa siku sita na hakuwa katika kiwango bora.
Yondani amekosa mechi nne dhidi ya Kagera Sugar, Azam, Singida United na Prisons ya Mbeya.