Ligi Kuu yanukia viporo

Dar es Salaam. Kuna kila dalili viporo vya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2019/2020 vikaanza mapema kuanzia mechi za mwanzoni za ligi hiyo kutokana na ushiriki wa timu nne nchini katika mashindano ya Klabu Afrika.

Licha ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutenganisha ratiba ya mechi za mashindano ya klabu Afrika na Ligi Kuu kwa muda wa siku tatu, kuna uwezekano mkubwa muda huo ukawa hautoshi kulingana na mahitaji ya maandalizi ya timu kwa ajili ya ushiriki katika michuano hiyo.

Wakati akitangaza tarehe ya kuanza Ligi Kuu msimu ujao juzi, Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura, alisema hakuna uwezekano kwa mashindano ya kimataifa na mengine kusababisha viporo kwa sababu wamezingatia suala hilo.

“Tunatoa angalizo hakutakuwa na upanguaji wa ratiba pasipo sababu ya msingi. Yale mambo ya timu kutuma maombi ya kupewa muda wa kujiandaa au kupumzika hatutayapa nafasi, “alisema Wambura.

Pengine kwa kuzingatia kalenda iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Bodi ya Ligi imepanga ratiba inayozipa nafasi ya kucheza siku tatu baada ya mechi za klabu Afrika timu zake zinazoshiriki mashindano ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Wambura, msimu wa Ligi Kuu 2019/2020 utaanza Agosti 23 kwa kuzikutanisha Simba na JKT Tanzania Uwanja wa Taifa. Huku Yanga ikifungua na Ruvu Shooting, Agosti 28 na Agosti 29, Azam itacheza na KMC.

Wakati huo ratiba ya mashindano iliyotolewa na CAF, ikionyesha mechi za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika zitacheza kati ya Agosti 23 hadi Agosti 25.

Kiporo cha kwanza cha ligi kinaweza kuwa cha Simba endapo itapangwa kuanzia hatua ya awali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani mechi zake zinadondokea tarehe ambayo itacheza mechi ya kwanza dhidi ya JKT Tanzania.

Ikiwa Simba itapangwa kuanza hatua ya awali, maana yake mechi yake dhidi ya JKT Tanzania italazimika kupangiwa tarehe nyingine na unafuu wake utakuja iwapo Simba itaanza raundi ya kwanza.

Lakini pamoja na hilo, licha ya utofauti wa siku tatu uliopo baina ya mechi za Azam, Yanga na KMC za mashindano ya Afrika na Ligi Kuu, bado zinaweza kupata viporo vya mapema.

Hilo linaweza kutokea iwapo, timu hizo zitaanzia ugenini kwa kupangwa kucheza na timu ambazo zinatoka kwenye nchi zisizo na usafiri wa ndege za moja kwa moja kutoka huko kuja Tanzania.

Ikiwa timu hizo zitapangwa kucheza Agosti 25 ugenini, zinaweza kujikuta zikitumia siku mbili kwa safari ya kurejea nchini na kuchelewa huko kunaweza kupelekea mechi zao za ligi kupangiwa tarehe nyingine

Changamoto nyingine ya ratiba ya ligi msimu ujao, ni uwepo wa mechi za Kombe la Mapinduzi mwezi Januari ambazo nazo zina uwezekano mkubwa wa kusababisha viporo.

Ratiba ya ligi inaonyesha mechi ya mzunguko wa kwanza kati ya Simba na Yanga itachezwa Januari 4, mwakani tarehe ambayo inaangukia muda ambao mashindano hayo huchezwa.

Kwa kawaida, mashindano ya Kombe la Mapinduzi, huanza mwishoni mwa Desemba na kumalizika Januari 13, hivyo mechi kati ya Simba na Yanga inaweza kusogezwa mbele na kupangiwa tarehe nyingine ili kupisha mashindanbo hayo iwapo zitashiriki kama ilivyo utamaduni wake.

Ukiondoa hilo, Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mujibu wa Wambura, itaanza Agosti 23 ikitanguliwa na mechi ya Ngao ya Jamii baina ya Azam na Simba itakayochezwa Agosti 17.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema ili ligi ionekane ya haki, lazima timu zote zicheze kwa wakati na kumaliza kwa wakati.

“Tutakuwa tunarudia makosa yaleyale kila siku kwa baadhi ya timu kuwa na viporo tena vingi, mfano msimu uliopita Yanga ilikuwa na haki ya kulalamikia viporo vya Simba,” alisema Rage.

Alisema haiwezekani Simba iwe na mechi Agosti 23 siku ambayo ratiba ya CAF pia inaanza kwani kuna uwezekano ratiba ya CAF ambayo Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa, itavuruga ratiba ya mechi yao ya Ligi.

Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Idd Kipingu alisema TFF na Bodi ya Ligi ilipaswa kabla ya kupanga ratiba iangalie kwanza ile ya CAF na Fifa.

“Tatizo sisi tuna haraka ya kupanga ratiba ya Ligi Kuu, hakuna utulivu katika upangaji wa ratiba ndiyo sababu mara kwa mara mechi zinaingiliana,” alisema Kipingu.