Maguli aanza kuzifumania nyavu Zambia

Tuesday October 8 2019

 

By THOMAS NG'ITU

Dar es Salaam. Mshambuliaji Elias Maguli ameanza kufanya vyema katika klabu yake mpya ya Nakambala Leopards kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wao 2-0 dhidi ya Kabwe YSA katika Ligi Kuu Zambia.
Maguli huu ni mchezo wake wa pili tangu ajiunge na klabu hiyo akiwa mchezaji huru.
Mshambuliaji huyu alikosa michezo mitatu ya kwanza baada ya kuchelewa kupata kibali cha kufanyia kazi nchini Zambia, lakini baada ya kupata nafasi ameonyesha makeke yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maguli alisema licha ya ushindani uliopo katika Ligi hiyo anaamini atafanya vizuri zaidi.
"Ligi ni ngumu lakini nitajitahidi kupeperusha bendera ya nchi yangu vizuri, pia kuisaidia timu yangu kukaa sehemu nzuri katika msimamo," alisema Maguli.
Magoli ya Maguli yameifanya timu hiyo kutoka nafasi ya 17 na kusogea mpaka nafasi ya 13, ikiwa na pointi baada ya kupoteza michezo mitatu, sare moja na ushindi mmoja.
Katika msimu uliopita akiwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara alikuwa akiichezea klabu ya KMC, lakini katika dirisha dogo aliachana na timu hiyo kwa kile kilichoelezwa kulikuwa na sintofahamu baina ake na uongozi.

Advertisement