Mama mzazi wa Guardiola afariki kwa corona

MAMA mzazi wa kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, Dolors Sala Carrio, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 huko Barcelona baada ya kupata maambuzi ya virusi vya corona.
Kwa vifo 637 vilivyotokea Jumatatu zimefanya waliopototeza maisha kutokana na virusi hivyo vya corona huko Hispania kufikia 13,055.
Mwezi uliopita, Guardiola alichangia Euro 1 milioni kusaidia mapambano ya janga hilo la virusi vya corona.
Pesa hiyo ilitumika kununua vifaa tiba na vifaa vya kujikinda kwa wauguzi wanaotoa huduma ya wale walioathirika waliopo kwenye hospitali. Barcelona ipo Catalonia, eneo ambalo linaripotiwa kuwa na idadi kubwa sana ya maambukizi ya virusi hivyo vya corona.
Guardiola, 49, amekuwa akiinoa Man City tangu Julai 2016 baada ya kufanya kazi Barcelona na Bayern Munich.
"Kila mtu anayehusika kwenye klabu ametuma ujumbe wake wa huzuni na kumjaza moyo katika kipindi hiki kigumu mwenzetu Pep, familia yake na marafiki," ilibainisha taarifa ya Man City iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii.
Manchester United nao walituma ujumbe wao kwenye mtandao wa kijamii na kuandika "tumehuzunishwa na taarifa hizi mbaya", na kuongeza: "Tunatuma rambirambi zetu kwa Pep na familia yake."