Mambo 4 yaliyoishusha daraja African Lyon

Dar es Salaam. Kabla haijapoteza mchezo dhidi ya Mbao kwa kufungwa mabao 3-1 ambao uliwashusha daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara hadi Daraja la Kwanza, ishara ya African Lyon kukutana na janga hizo zilijionyesha mapema tangu mzunguko wa kwanza msimu huu.

Kipigo hicho kiliifanya African Lyon kubaki na pointi 22 ambazo zinaifanya isiweze kufikia timu yoyote katika msimamo wa ligi hata kama itaibuka na ushindi katika mechi tatu zilizobaki.

Timu hiyo katika michezo 35 iliyocheza imefungwa mabao 21, imetoka sare mara 10 na imeshinda michezo minne pekee ya Ligi Kuu.

Matatizo na changamoto mbalimbali ambazo ziliikabili African Lyon kabla Ligi Kuu kuanza, vimechangia kuishusha mapema huku zikiwa zimebaki raundi chache kabla ya ligi kumalizika.

Mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi, usajili dhaifu, ukata na mazingira yasiyokuwa rafiki kwa wachezaji ni mambo manne yaliyoiangusha African Lyon msimu huu.

Benchi la ufundi

Mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha iliyofanya kuanzia mwanzoni mwa msimu, yamechangia kuiathiri timu hiyo kiufundi kwani makocha hao kila mmoja alileta mbinu mpya katika kikosi.

African Lyon ilianza kunolewa na Kocha Mfaransa, Soccoia Lionel lakini ndani ya msimu ililazimika kubadili makocha mara nne bila mafanikio.

Soccoia aliyekuwa na mipango ya kuifanya timu hiyo kuwa ya ushindani, hakudumu aliondoka kutokana na ukata na nafasi yake ilichukuliwa na Adam Kipatacho aliyekuwa msaidizi wake.

Hata hivyo, Kipatacho naye hakudumu na sababu za kuondoka kwake hazikuwekwa wazi na timu hiyo ilitua mikononi mwa Suleiman Jabir.

Jabir naye hakudumu, aliondoka na uongozi ulimpandisha aliyekuwa msaidizi wake, Salvatory Edward kuwa kocha mkuu mpaka sasa.

Usajili dhaifu

African Lyon ilianza mechi za ligi ikiwa haina kikosi imara cha ushindani baada ya kufanya usajili wa zimamoto kwa ajili ya msimu huu.

Klabu hiyo ilisajili wachezaji katika mazingira magumu hatua iliyochangia kupeleka majina ya wachezaji wake muda mfupi kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Ukata

Jambo jingine lililoiangusha timu hiyo ni ukata uliochangia kushusha morali na hamasa kikosini kutokana na wachezaji kutopata stahiki na huduma nzuri.

Licha ya kubadili makocha mara kadhaa, mtikisiko wa uchumi kwenye klabu umetajwa kuwa moja ya sababu zilizochangia kuishusha timu hiyo.

Akizungumzia hilo, mmiliki wa African Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ alisema alaumiwe yeye kwa matokeo mabaya iliyopata African Lyon.

“Kila mtu aliona namna ligi ilivyokuwa na changamoto, lakini yote kwa yote nabeba lawama zote mimi asilaumiwe yoyote,” alisisitiza Kangezi.

Alisema kuyumba kwa uchumi kulichangia kwa kiasi kikubwa wachezaji kucheza chini ya kiwango kwa kuwa hawakuwa na morali na alidai alifanya usajili uliokidhi viwango kabla ya kuanza mashindano hayo.

Mazingira magumu

Wakati Kangezi akitaka lawama apewe yeye, Edward alisema licha ya changamoto mbalimbali, lakini mazingira ya ligi yalikuwa kikwazo.

“Timu ilikuwa na changamoto ya uchumi, hivyo tulipokwenda kucheza mkoani tulilazimika kupunguza muda wa safari ili kuokoa gharama. Wachezaji walikosa muda wa kurejesha viwango,” alisema kocha huyo.

Alisema ingawa wachezaji hawakuwahi kukosa chakula katika kipindi chote wanapokuwa kambini, lakini posho zao zilichelewa kwa kuwa ligi haina mdhamini.

Mchambuzi Kenny Mwaisabula alisema hali ya kiuchumi umeiathiri African Lyon. “Lyon si timu mbaya imeshuka kutokana na hali yake, mfumo wa nchi yetu kwenye ligi ni mgumu tofauti na wenzetu Ulaya,” alisema Mwaisabula.