Mane, Bakambu bado waongoza kwa ufungaji Afcon

Muktasari:

Washambuliaji hao kutoka Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameshazifungia nchi zao mabao matatu kila mmoja katika fainali zinazoendelea Misri za Mataifa ya Afrika.

Mshambuliaji hatari wa Liverpool Sadio Mane na nyota wa klabu ya Beijing Guoan, Cedric Bakambu ni kati ya wachezaji watatu wanaoongoza kwa ufungaji magoli katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea nchini Misri.
Mane, anayeichezea Senegal, na Bakambu (Congo DR) wameshafunga mabao matatu kila mmoja sawa na Adam Ounas (Napoli) anayeichezea Algeria.
Mane na Ounas wana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao baada ya timu zao kufuzu kucheza nusu fainali wakati Bakambu atakuwa akiwashuhudia wenzake baada ya Congo kutolewa katika hatua ya 16 bora.
Watatu hao wanafuatiwa na lundo la wachezaji waliofunga mabao mawili kila mmoja, akiwemo mshambualiaji anayeondoka klabu ya Simba, Emmanuel Okwi ambaye aliifungia Uganda mabao mawili kabla ya kutolewa katika 16 bora.
Wengine ni Belaili, Mahrez (Algeria), Elmohamady, Salah (Misri), Kodjia, Zaha (Ivory Coast), Andriamahitsinoro (Madagascar), J. Ayew (Ghana), Bahoken (Cameroon), En-Nesyri (Morocco), Msakni (Tunisia), Okwi (UGA), Olunga (Kenya), Pote (Benin), Yattara (Guinea) na Zungu (Afrika Kusini)