Mbao FC yaunda kamati kujinusuru Ligi Kuu

Tuesday March 13 2018

 

By Saddam Sadick

Kutokana na kusuasua kwa Mbao FC kwa kushindwa kupata matokeo mazuri, uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi kuwa tayari umekaa na kuunda mkakati wa jinsi watakavyoshinda mechi zilizobaki ili waweze kubaki Ligi Kuu.

Mbao ambayo imepoteza mechi 11 hadi sasa, imekusanya pointi 19 na kukaa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, ambapo wadau wa soka jijini Mwanza wameanza kuwa na wasiwasi kwa timu hiyo juu ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Daniel Naila alisema kuwa bodi ya timu ilikutana Jumamosi iliyopita na moja ya azimio lao ilikuwa ni kuunganisha nguvu ya kuinusuru timu kubaki Ligi Kuu.

Alisema kuwa timu haina mgogoro mkubwa, isipokuwa ni mambo ya kutofautiana kimawazo baina ya viongozi na wajumbe, lakini mambo ni mazuri na timu itabadilika.

“Bodi ya Mbao ilikutana Jumamosi na mambo yaliyoafikiwa ni kuunganisha nguvu ya pamoja kuhakikisha timu inabaki Ligi Kuu,kuhusu migogoro,hakuna kabisa,labda ni ile hali ya kutofautiana mawazo baina ya viongozi na wajumbe na utamaduni wetu ni kumaliza mambo ya Mbao kwa ndani”alisema Naila.

Katibu huyo aliongeza kuwa kuhusu madai ya mishahara kwa wachezaji, tayari menejimenti imeshakaa nao na kuafikiana kulipwa mwishoni mwa mwezi huu na kwamba madai yao ni miezi miwili na si mitatu kama inavyosemekana.

Alisisitiza kuwa hakuna mchezaji yeyote ambaye ameshalipwa mshahara na kuwaacha wengine kama inavyodaiwa na kusema kuwa hiyo haiwezi na haitatokea ndani ya timu yao.

“Ni kweli wachezaji wanadai mishahara yao ya miezi miwili na siyo mitatu na uongozi umekaa nao na kukubaliana kuwamalizia mwishoni mwa mwezi wa tatu, lakini hakuna cha kwamba kuna ambaye amelipwa na wengine kuachwa, naomba hili lieleweke halijawahi kutokea,” alisisitiza katibu huyo.

Advertisement