Mbao FC yapata pigo

WAKATI uongozi wa Mbao FC ukiwa kwenye mipango ya kuanza kuwaongeza mikataba wachezaji wao, kipa Kelvin Igenderezi ameachana na timu hiyo.
Igenderezi amemaliza mkataba na timu hiyo ambapo sasa amejiunga na Pamba FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Ujio wa kipa huyo umefanya Pamba FC  sasa  kuwa na makipa watatu ambao ni Deus Mwakigo na Ally Ramadhani jambo ambalo litafanya kuwepo na ushindani mkali wa namba kwenye nafasi hiyo.
Afisa Habari wa Klabu hiyo, Johnson James amesema Igenderezi amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Pamba.
Alisema uamuzi wa kuwa na makipa matatu ni baada ya msimu uliopita kuwa na makipa wawili ambapo mmoja baadaye alipata majeraha na kubaki na kipa mmoja tu.
“Tumefunga usajili na makipa maana tumefikisha watatu, hapo ni kupambana kugombania namba kwani wote ni makipa wazuri, hapo pia ni jukumu la kocha kuona nani mzuri zaidi,” anasema James.
Kwa upande wa Igenderezi alisema ataonyesha makali yake kama alivyokuwa Mbao FC hivyo hana wasiwasi juu ya kupata namba kikosi cha kwanza.
“Kikubwa naomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki na wachezaji wenzangu, nimekuja kwa lengo moja la kuipa mafanikio hii timu na kurudisha heshima yake waliyojiwekea miaka ya nyuma,” alisema Igenderezi.