Messi aweka rekodi Hispania

Monday January 14 2019

 

Madrid, Hispania. Nahodha wa Barcelona, Lionel Messi amezidi kuchanja mbuga, baada ya kufunga bao la 400 katika mashindano ya Ligi Kuu Hispania.

Messi alifikia rekodi hiyo alipofunga bao katika mchezo  wa ligi dhidi ya Eibar, uliochezwa kwenye Uwanja wa Nou Camp, Hispania.

Mabao mawili yalifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay Luiz Suarez aliyefikisha 13 msimu huu.

Messi anakuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 400  katika ligi tano bora Ulaya akiwa na wastani wa kufunga bao la kwanza miaka 14 iliyopita.

Mwaka 2005 alifunga bao la kwanza, alipopewa pasi ya mwisho na nyota wa zamani wa Brazil Ronaldinho.

Barcelona inaongoza kwa pointi tano mbele ya Atletico Madrid inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Lig Kuu Hispania.

Mpinzani wake wa muda mrefu Cristiano Ronaldo ana mabao 409 aliyofunga katika mechi 507 tofauti.

Nahodha huyo wa Ureno, amefunga mabao hayo katika ligi tatu tofauti England, Hispania na Italia akiwa Manchester United, Real Madrid na Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin.

Ronaldo amefunga mabao 311 katika mechi 292 alizocheza Hispania kabla ya kutimkia Italia akiwa na miaka 33.

Mshambuliaji wa Athletic Bilbao, Thelmo Zarra, anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao 251 katika mechi 277 alizocheza Hispania.

Advertisement