Advertisement

Mpango wa Ligi Kuu ya Ulaya wakosolewa

Wednesday October 21 2020
ligi kuu pic

London, Ungereza. Pendekezo la kuanzishwa kwa Ligi Kuu ya soka barani Ulaya itakayojumuisha klabu vigogo tu na ambalo linaungwa mkono na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), limekosolewa na La Liga na makundi ya mashabiki.
Taarifa ya kituo cha televisheni cha Sky jana Jumanne ilidai kuwa majadiliano ya mpango huo yanakaribia kukamilika. Mpango huo unapendekeza kuanzishwa kwa Ligi Kuu ya Ulaya itakayojumuisha klabu 18, huku mwishoni mwa msimu kukiwa na mechi za mtoano.
Ligi hiyo itajumuisha vigogo wa soka Ulaya kama Real Madrid, Barcelona, Liverpool, Manchester United na Bayern Munich.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mpango huo utapata dola 6 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh13 trilioni za Kitanzania) kutoka benki kubwa kuhusiana na mapato ya mikataba ya haki za televisheni.
Kila klabu itakayoshiriki itapata "maelfu ya pauni za Kiingereza ili zishiriki".
Ligi Kuu ya Ulaya imekuwa ikiaminiwa kuwa ndio njia kubwa ya klabu vigogo kuongeza fedha katika mapato yao, lakini kuanzishwa kwake kutaathiri Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na ligi kuu za nchi wanachama.
Ingawa taarifa hiyo inadai kuwa mapendekezo hayo yatazifanya klabu kuendelea kushiriki katika ligi za nchi na michuano ya Ulaya katikati ya wiki, mpango huo utaongeza shughuli katika kalenda ambayo imeshazongwa na mechi nyingi.
"Hii mipango 'ya chinichini' huonekana mizuri pale tu inapopangwa baa saa 11:00 alfajiri," alisema rais wa La Liga, Javier Tebas.
"Wabunifu wa wazo hilo -- kama kweli wapo kwa sababu hakuna anayelitetea -- si tu wanaonyesha kutokuwa na uelewa wa uendeshaji na utamaduni wa soka la Ulaya na ulimwenguni, lakini pia hawajui masuala ya masoko ya haki za televisheni.
"Mradi wa aina hii utamaanisha athari kubwa za kiuchumi kwa waandaaji na taasisi zinazotoa fedha."
Kuvuja kwa mapendekezo ya mageuzi hayo ya soka, kumekuja zaidi ya wiki moja tangu mpango ya Liverpool na Manchester United wa "Project Big Picture" wa kufanya mageuzi katika Ligi Kuu ya England ukataliwe na klabu.
Mpango huo ulilenga kupunguza idadi ya timu za Ligi Kuu hadi 18 na kufuta michuano ya Kombe la Ligi ili kutoa nafasi kwa michuano ya Ulaya.

Advertisement