Mshambuliaji wa Yanga, avunjika mguu akimbizwa hospitali Bugando yuko njiani kuletwa Muhimbili

Wednesday October 23 2019

 

By Khatimu Naheka na Majuto Omary

Dar es Salaam. Mshambuliaji Yanga, Maybin Kalengo huenda asicheze mechi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pryamids baada ya kuumia mguu na kukimbizwa hospitali ya Bugando kwa matibabu anatarajiwa atasafirishwa kwa ndege kuja Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Kalengo aliumia baada ya kugongana na kipa wa Pamba na kusababisha penalti iliyofungwa na Patrick Sibomana katika ushindi huo wa mabao 2-1 iliyopata Yanga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Pamba leo asubuhi kwenye Uwanja CCM Kirumba, Mwanza.

Kalengo alionekana kupata maumivu makali na kulazimika kutolewa na kukimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.

Daktari wa Yanga, Sheck Mngazija alisema kuwa baada ya huduma ya kwanza, Kalengo atasafirishwa kwa ndege kwa ajili ya matibabu zaidi katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Ni kweli kuwa ameumia na hatacheza mechi dhidi ya Pyramid, jana alikuwa katika benchi wakati timu yake ikicheza na Mbao FC katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara,”alisema Mngazija.

Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa kutokuwepo kwa Kalengo ni pigo kwa Yanga kwani ni miongoni mwa wachezaji tegemezi katika timu yao.

Advertisement

“Si unajua kuwa Molinga (David) hana leseni ya kucheza mechi hiyo na Kalengo ni miongoni mwa wachezaji ambao walitarajiwa kuwa katika mstari wa ushambuliaji pamoja na Sadney Urikhob, Juma Balinya, Mrisho Ngassa, Papy Kambamba Tshishimbi na Mapinduzi Balama,” alisema Bumbuli.

Katika mchezo huo bao la pili likifungwa na Juma Balinya akimalizia pasi ya kiungo Deuse Kaseke.

Pamba inayoshiriki Ligi daraja la kwanza ilipata bao la kufutia machozi lililofungwa kwa kichwa Rashid Njete akimalizia krosi ya Maka Miraji.

Katika mchezo huo kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera aliwatumia wachezaji wengi ambao hawakupata muda wa kutosha katika mchezo wa jana dhidi ya Mbao waliyoshinda bao 1-0 kwenye uwanja huo.

Advertisement