Raptors wapoteana mwishoni kwa Bucks Fainali za Kanda NBA

Thursday May 16 2019

 

By Matereka Jalilu

Licha ya kuongoza kwa muda mrefu na kuwatawala kwenye robo tatu za kwanza,Toronto Raptors alfajiri ya leo Alhamisi wamejikuta wakipigwa na Milwaukee Bucks kwenye mchezo wa kwanza fainali ya ukanda wa mashariki.

Raptors inayoongozwa na Kawhi Leonard ilishindwa kumalizia mchezo kwenye robo ya mwisho na kuwaruhusu wapinzani wao Bucks wakishinda mchezo huo.

Baada ya kuipeleka fainali ya ukanda wa Mashariki kwa kufunga kikapu cha sekunde ya mwisho mchezo wa saba dhidi ya Philadelphia 76ers, Kawhi leo alishuhudia timu yake ikipoteza mchezo huo huku Kyle Lowry akiwa na mchezo bora zaidi kwa kufunga jumla ya pointi 30.

Kichapo cha Raptors kilitokana na kufunga vikapu 17 pekee kwenye robo ya nne wakati Milwaukee iliyobebwa na mchezaji Brook Lopez aliyefunga pointi 3 mara nne na kufanikiwa kufunga jumla ya vikapu 29 na kuipa ushindi Bucks wa 108-100.

Katika ukanda wa Magharibi,Golden State Warriors wao baada ya kuwa na kazi pevu ya kuwaondoa wapinzani wao wakubwa Houston Rockets wanacheza fainali ya nne mfululizo ukanda huo na wana kazi nyepesi dhidi ya Portland Trail Blazers ambayo ilifika fainali kwa kuwaondoa Denver Nuggets.

Mchezo wa kwanza baina yao uliochezwa juzi,Warriors waliibuka na ushindi wa 116-94 ambapo mchezo ujao wa pili utachezwa saa 10  alfajiri ya Ijumaa.

 

Advertisement