Ronaldinho aachiwa kwa dhamana

Muktasari:

  • Ronaldinho (40), aliyewahi kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia mara mbili alisafiri kuingia Paraguay kunadi kitabu chake na kampeni ya kuwasaidia watoto wasio na msaada kabla ya kunaswa kwa kufoji nyaraka.

MSHINDI wa Kombe la Dunia, Ronaldinho Gaucho ameachiwa kwa dhamana kutoka gerezani nchini Paraguay baada ya kukaa kwa siku 32 kwa kosa la kuingia nchini humo na pasipoti bandia.

Pasipoti ya nyota huyo wa zamani wa Brazil ambaye majina yake Ronaldo de Assis Moreira aliyotumia kuingia nchini humo, inaonyesha jina lake sahihi, mahali alipozaliwa na siku ya kuzaliwa lakini inaonyesha kwamba ni raia asili wa Paraguay.

Ripoti zaidi zilionyesha Ronaldinho pamoja na kaka yake, walilipa dhamana ya pauni milioni 1.3 na wataruhusiwa kurejea Hoteli ya Palmaroga, mjini Asuncion.

Katika hoteli hiyo ndipo ambapo awali walishikiliwa na Polisi waliokuwa wakifanya msako.

Nyota huyo wa zamani wa FC Barcelona hatoruhusiwa kuondoka nchini humo hadi pale ambapo kesi yake itakapomalizika.

Julai mwaka jana, Gaucho aliripotiwa kuwa pasipoti zake za Brazil na Uhispania zilichukuliwa kwa kutolipa ushuru.

Ronaldinho aliyenyakua tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mwaka 2004 na 2005, alifurahia soka lake akiwa na FC Barcelona kabla ya kwenda Italia kumalizia soka lake la ushindani akiwa na AC Milan.

Pia ni mmoja wa nyota walioshinda Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa na kikosi cha Brazili sambamba na nyota wenzake akiwemo Ronaldo na Rivaldo.