Samatta kufanyiwa vipimo, baba afunguka

Muktasari:

Samatta amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England na sasa Aston Villa wameonyesha kuwa siriasi zaidi kutaka huduma yake.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Mbwana Samatta yuko njiani kwenda jijini Birmingham, Uingereza kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya tayari kwa kujiunga na klabu mpya ya Aston Villa.
Samatta ameondoka jijini Genk, Ubelgiji, leo Ijumaa kwenda England kukamilisha dili la kujiunga na Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baba mzazi wa supastaa huyo, Mzee Ally Pazi Samatta amesema amezungumza na mwanae muda mfupi akiwa uwanja wa ndege nchini Ujerumani tayari kwa safari ya Uingereza.
Kikosi cha KRC Genk kipo nchini Ujerumani kwa ajili ya maandalizi ya mechi zake za Ligi Kuu Ubelgiji maarufu kama Jupiler Pro ambayo ilisimama kwa muda.
"Amenipigia simu kama saa moja iliyopita na kunitaarifu kwamba, yuko safari kwenda Uingereza kufanyiwa vipimo na baadaye kukamilisha mipango mingine.
"Nimejikuta natokwa na machozi ya furaha, kubwa namuombea kwa Mungu amfanyie wepesi katika hatua aliyofikia ili atimize ndoto zake za kucheza Ligi Kuu ya England," amesema.
Mara baada ya uhamisho huo kukamilika, Samatta, ambaye ameifungia Genk jumla ya mabao 76 tangu ajiunge nayo akitokea TP Mazembe ya DR Congo, atakuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza Ligi Kuu England.
Habari ambazo zimepatikana hivi karibuni zinaeleza kuwa, mchakato wa Samatta kupata kibali cha kazi umekamilika hivyo anaweza kuanza kuitumikia Aston Villa kwenye mchezo wa kesho Jumamosi.