Senegal, Algeria hesabu tupu

Friday July 19 2019

 

By Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Hesabu sahihi na mbinu za makocha Aliou Cisse wa Senegal na Djamel Belmadi zina nafasi kubwa ya kuamua mechi ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), leo baina ya timu hizo jijini Cairo.

Ubora ulioonyeshwa na timu zote mbili katika hatua zilizopita za mashindano hayo sambamba na kiu ya kila upande kutwaa ubingwa, ni mambo mawili yanayotoa taswira ya ugumu wa mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, kuanzia saa 4.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Ni mechi ambayo inazikutanisha timu mbili ambazo aina ya soka lao linaendana, ambalo ni lile la kushambulia kwa kulazimisha muda mwingi kuwa eneo la timu pinzani, likichagizwa na uimara na nidhamu ya hali ya juu katika safu zao za ulinzi ambazo zimekuwa zikiwahi kwa haraka kurudi jirani na lango pindi wanaposhambuliwa.

Na kwa kudhihirisha hilo, mataifa hayo yapo katika kundi la timu tatu zilizofunga idadi kubwa ya mabao kwenye fainali hizo ambapo Algeria inaongoza ikipachika 12 wakati Senegal inashika nafasi ya tatu ikiwa imefunga manane.

Lakini hata kwenye ulinzi, zina rekodi nzuri kwani Senegal ndiyo imefungwa mabao machache ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja, huku Algeria ikifungwa mabao mawili.

Kwa timu hizo kunolewa na makocha wazawa, fainali baina yao inakuwa ya tano kwenye fainali za Afcon kuzikutanisha timu zinazonolewa na makocha wazawa.

Advertisement

Fainali nne zilizopita ambazo zilikutanisha makocha wazawa ni Ethiopia dhidi ya Misri mwaka 1962, Ghana na Tunisia 1965, Ghana dhidi ya Uganda mwaka 1978 na nyingine ni ile ya mwaka 1998 ya Misri na Afrika Kusini.

Mbali na hilo, makocha hao wawili wameweka rekodi ya kuongoza timu kutinga hatua ya fainali, huku wakiwa wamewahi kushiriki mashindano hayo wakiwa wachezaji - tena manahodha.

Cisse amecheza Afcon mwaka 2002 na 2004 akiwa nahodha wa Senegal kama ilivyo kwa Belmadi aliyekuwa nahodha wa kikosi cha Algeria mwaka 2004 kiliposhiriki mashindano hayo.

Tangu wacheze mechi zao za kwanza kwenye hatua ya makundi ya Afcon mwaka huu, hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa Senegal imeongoza kwa kupiga mashuti - ikipiga 75 dhidi ya 71 ya Algeria.

Katika mashuti hayo, mashuti 26 ya Senegal yalilenga lango wakati mashuti ya Algeria yaliyolenga lango la wapinzani ni 25.

Hadi inatinga fainali Senegal imepiga kona 33 na Algeria imepata kona 21, huku ikilingana kwa kuotea ikifanya hivyo mara 14.

Idadi ya faulo ni 118 kwa Senegal na 132 kwa Algeria, huku kadi za njano zikitolewa nane kwa wachezaji wa Senegal na 10 kwa wale wa Algeria huku kukiwa hakuna kadi nyekundu.

Kwa kocha Cisse hata akishindwa kutwaa taji atakuwa amemaliza mashindano akiwa na rekodi tamu ya kushiriki michuano mikubwa miwili duniani inayohusisha timu za Taifa - akiwa kocha na mchezaji.

Nyota huyo wa zamani katika soka ameshiriki Kombe la Dunia mwaka 2002 akiwa mchezaji na 2018 akiwa kocha, na pia ameshiriki Afcon 2002 na 2004 akiwa mchezaji na mwaka huu akiwa kama kocha.

Katika hali inayoleta mshangao, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa mara nyingine limefanya mabadiliko ya mwamuzi atakayechezesha fainali hiyo.

Awali, CAF ilipanga mwamuzi Bemlek Tessema Weyessa kutoka Ethiopia kabla ya kumbadili na kumpanga Victor Gomez wa Afrika Kusini, lakini juzi ghafla likafanya mabadiliko na kumpanga Sidi Alioum (36) kutoka Cameroon.

Mwamuzi huyo atasaidiwa na Evarist Menkouande na Nguegoue Elvis Guy Noupue - wote kutoka Cameroon - wakati mwamuzi wa akiba atakuwa ni Eric Otogo-Castane wa Benin.

Senegal inasaka ubingwa wake wa kwanza kwenye fainali hizo baada ya kukosa mwaka 2002 ilipochapwa na Cameroon kwa mikwaju ya penati 3-2, wakati Algeria inasaka ubingwa wake kwa mara ya pili baada ya kutwaa taji hilo mwaka 1990.

Mchezo huo pia utashuhudia vita ya wachezaji wawili nyota, Sadio Mane wa Senegal na Adam Ounas ambao kila mmoja atakuwa na kibarua cha kufunga mabao ili amfikie na kumpita kinara Idion Ighalo wa Nigeria mwenye mabao matano, ikizingatiwa kwamba kila mmoja amepachika mabao matatu hadi sasa.

Advertisement