Shehena ya malori ya dawa yakabidhiwa Muhimbili

Tuesday August 13 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Bohari ya Dawa (MSD) nchini Tanzania imekabidhi dawa, vifaa na vifaa tiba kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa ajili ya kuwahudumia majeruhi wa ajali ya moto waliohamishiwa hospitalini hapo kutoka mkoani Morogoro.

Kwa mujibu wa MSD, makabidhiano hayo ya dawa ni mwitikio wa maombi ya dharura yaliyoombwa na MNH kwa ajili na majeruhi hao.

Majeruhi hao ni wale walionusurika katika ajali ya lori la mafuta ya petroli lililoangika kisha kulipuka eneo la Msamvu Mkoa wa Morogoro Jumamosi iliyopita ya Agosti 10, 2019 ambapo hadi jana Jumatatu jioni, waliokuwa wamefariki kutokana na ajali hiyo ni 75 na majeruhi zaidi ya 50.

Meneja wa MSD, Kanda ya Dar es Salaam, Celestine  Haule amesema mpaka leo Jumanne Agosti 13,2019 jumla ya shehena ya malori matano yameshakabidhiwa Muhimbili zikiwemo dawa muhimu zinazotumika kwa ajili ya kuokoa maisha ya majeruhi hao.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu amesema malori ya shehena za dawa, vifaa na vifaa tiba yalikabidhiwa jana Jumatatu na leo wanatarajia kupeleka dawa zingine.

Advertisement