Simba yaifyeka Mlandege bao 1-0, Niyonzima ang'ara

Tuesday January 8 2019

 

Timu ya Simba imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Visiwani Zanzibar leo Jumanne usiku.

Bao pekee la Simba lililofungwa na Haruna Niyonzima wa Simba katika mechi yao ya mwisho ya makundi ya kombe la Mapinduzi, liliifanya Simba kuibuka na ushindi huo ambao wamefikisha alama 9 na kuongoza kwenye Kundi A.

Tangu asajiliwe Simba, zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa,  kiungo huyo raia wa Rwanda hajawahi kuifungia timu yake bao lolote kwenye mashindano ambayo Simba imeshiriki.

Niyonzima amekuwa mchezaji ambaye hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara ukiachana na msimu wake wa kwanza ambao alikaribishwana majeruhi yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Bao hilo ambalo lilifungwa dakika ya 21 lilitokana na mchezaji wa Mlandege FC, Ali Hamidu aliyemchezea rafu Asante Kwasi eneo la hatari na kusababisha penalti.

Katika kipindi hicho cha kwanza mchezaji wa Mlandege, Hamidu alishindwa kuendelea na mchezo huo baada ya kuumia goti ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Fini Salum.

Hamidu aliwahishwa hospitali baada ya kushindwa kutembea huku akiugulia maumivu ya goti.

Advertisement