Simba yapania yamleta mshambuliaji Mkongo, watano kufyekwa

Tuesday March 24 2020

 

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck akiwasilisha ripoti yake na mapendekezo ya nyota gani anaowataka, imefahamika mabosi wa klabu hiyo wameanza mipango ya kukisuka upya kikosi chao wakilenga michuano ya CAF na wamemfuata mchana nyavu matata nchini DR Congo.
Taarifa ambazo zimepenyezwa kwa Mwanaspoti na kuthibitishwa na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo ni kwamba Kocha Sven amependekeza aletewe mashine za kufunga mabao na fasta mabosi hao wameanza mchakato wa kusaka mastraika kabla ya kuwachuja kupata atakayefaa.
Mmoja ya mastraika wanaotajwa kutaka kuvutwa Msimbazi na ambaye yupo kwenye mazungumzo na kama kila kitu kitaenda sawa, atatua jumla bila mchujo kutokana na uwezo wake katika kufunga mabao, ni Mpiana Mozizi anayekipiga katika klabu ya FC Lupopo ya DR Congo.
Mozizi ni mmoja wa wafungaji watatu wanaoongoza mabao katika ligi ya nchi hiyo kwa sasa, wakifunga mabao 12 kila mmoja, jambo lililowashawishi mabosi wa Simba kutaka kumvuta Msimbazi ili ashirikiane na Meddie Kagere kufanya mambo kwenye ligi ya ndani na ile ya Afrika.
Straika huyo anachuana vikali kwa sasa na nyota wa TP Mazembe, Jackson Muleka na Fiston Kalala wa AS Vita katika ufungaji mabao kwenye ligi ya DR Congo na mmoja wa mabosi wa Simba ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Klabu, ndiye anayesimamia mazungumzo na straika huyo na wiki iliyopita tu wametoka kuzungmzia mambo ya msingi kuhusu maslahi binafsi.
Mozizi anayetajwa kuwa na umri wa miaka 27 anajulikana katika soka la DR Congo kwa umahiri wake sio kwa kufunga tu, bali pia nguvu na akili alizonazo wakati anapokabiliana na mabeki na ana uwezo wa kufunga kwa mabao ya miguu yote na hata kwa kichwa kutegemea nafasi.
Mwanaspoti imezungumza na straika huyo na kuthibitisha kwa sasa anasubiri jibu la bosi huyo wa Simba (jina tunalo) ili kuamua hatima yake kwa msimu ujao baada ya mazungumzo yao ya awali kwenda vizuri.
“Walinifuata Simba muda mrefu sasa tangu tumezungumza na wiki iliyopita walitaka kujua nahitaji kiasi gani nimewaambia wakiweza kufikia hapo naweza kuja, muulize huyu bosi (anamtaja) anajua wamefikia wapi,” alithibitisha Mozizi na kuongeza;
“Mimi ni mchezaji siogopi kucheza kokote najua Simba ni klabu kubwa hapo Tanzania najua kuna rafiki yangu pale ambaye ni kaka yangu Deo Kanda ananifahamu nitafurahi kama nitaungana naye hapo.”

MSIERRA LEONE NAYE YUMO
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amethibitisha kupokea ripoti na mapendekezo ya kocha wao, Sven kuhusu wachezaji gani anaowataka kuimarisha kikosi na kwamba kuna mastraika wawili wanaofuatiliwa kwa ukaribu mbali na huyo Mozizi.
Mshambuliaji wa kwanza anayetajwa anakipiga Al Jandal ya Ligi Kuu Saudi Arabia, Sheka Fofanah raia wa Sierra Leone anayemilikiwa na kampuni ya Heritage Soccer huku msimamizi wake akiwa ni Samuel Joel.
Fofanah alisajiliwa na Al Jandal mwaka 2020, akitokea Al-Mina’a ya Iraq na mpaka sasa ameifungia timu yake bao moja katika mechi nne alizocheza huku mkataba wake ukitarajiwa kumaliza Mei mwaka huu.
Joel alithibitisha Simba kumtaka Fofanah ambaye kampuni yao inamsimamia Kocha wa Yanga, Luc Eymael na nyota wakali akiwamo Juan Makusu.
“Tumefanya sana biashara hapo Tanzania ikiwamo Pascal Wawa aliyepo Simba, na pia tulihusika kumleta Eymael Yanga, na tunatamani Fofanah aje huko, ila mambo yamesimama kwa sababu ya Corona,” alisema Joel aliyefichua Yanga na Azam pia zinamtaka nyota huyo.
Mbali na Fofanah, straika mwingine anayenyemelewa na Simba ni Reliants Lusajo mwenye mabao 11 mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara sambamba na kiungo wa timu hiyo, Lucas Kikoti.
Kwa upande wa mabeki ambao kocha Sven amemtaja katika mapendekezo yake ni Bakar Nondo Mwamnyeto wa Coastal Union.
Senzo alisema wanachokifanya sasa ni  kufanya skauti katika maeneo mbalimbali ya Afrika ili kupata wachezaji wa maana na si kila mchezaji ambaye wanawasiliana naye au kumfuatilia ndio huyo huyo watamsajili bali watawasajili wachache kati ya wengi.
“Kocha ametupatia maeneo anayotaka yaongezwe nguvu na si kutupatia majina ya wachezaji ambao anawataka kwa maana hiyo tumeingia sokoni kulingana na bajeti yetu ambavyo itakuwa nadhani tutasajili na kupata wachezaji waliokuwa bora msimu huu,” alisema Senzo.

WATANO WATEMWA
Aidha habari za ndani kutoka Simba zinasema wachezaji watano ndani ya kikosi cha sasa wapo hatarini kupigwa panga mwisho wa msimu kutokana na ripoti iliyoachwa na Sven.
Wachezaji hao ni; Said Ndemla, Yusuph Mlipili ambao mikataba yao inamalizika, Mbrazili Tairone Santos, Rashid Juma na Kennedy Juma ambao, hawajamridhisha kocha Sven.

Advertisement