Simba yaweka rekodi Afrika

Monday January 14 2019

 

By Charles Abel,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mechi tatu ilizocheza nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, zimetosha kuthibitisha Simba makali ya safu yake ya ushambuliaji kwenye mashindano hayo.

Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano hayo juzi, sio tu umeendeleza ubabe wa Simba nyumbani msimu huu lakini pia umedhihirisha kuwa una moja ya safu kali.

Licha ya uwepo wa timu tishio na ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu, safu ya ushambuliaji ya Simba imezifunika klabu hizo zote kwa kuwa timu inayoongoza kupachika idadi kubwa ya mabao katika mechi ambazo kila timu imeshacheza hadi sasa.

Katika mechi tano ambazo imeshacheza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikianzia kwenye mechi za awali, Simba imefunga jumla ya mabao 15 ambayo ni wastani wa mabao matatu kwenye kila mchezo ambao imecheza ikifuatiwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini ambayo yenyewe imefunga mabao tisa tu huku Wydad Casablanca ya Morocco na Horoya ya Guinea zenyewe kila moja ikiwa imefunga mabao nane.

Makali ya safu ya ushambuliaji ya Simba yalianzia kwa ushindi wa mabao 4-1 ilioupata nyumbani dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatini kwenye mechi ya hatua ya awali ya mashindano hayo kabla ya kwenda kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 ugenini huko Manzini, Eswatini.

Hatua iliyofuata Simba ilianza ugenini dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia ambapo ilifungwa mabao 2-1 lakini ikageuka kuwa mbogo kwenye mchezo wa marudiano nyumbani ilipoibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 ambayo yaliwavusha na kuingia hatua ya makundi, ikipangwa sambamba na timu za JS Saoura, Al Ahly ya Misri na AS Vita Club kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

Ukiondoa kuwa timu iliyofunga idadi kubwa ya mabao kwenye mashindano hayo hadi sasa, kwa kudhihirisha kuwa safu yao ya ushambuliaji imekuwa haifanyi ajizi katika kufumania nyavu, kati ya mabao hayo 15 iliyoyafunga hadi sasa, 10 yamefungwa na nyota wake watatu ambao hucheza nafasi ya ushambuliaji ambao ni Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco.

Kagere ndiye kinara wa Simba katika kufumania nyavu kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na hadi sasa ameshapachika mabao matano yanayomfanya ashike nafasi ya pili kwenye chati ya jumla ya ufungaji bora ya mashindano hayo nyuma ya Moataz Al-Mehdi wa Al Nasr ya Libya mwenye mabao saba.

Mshambuliaji wa Simba anayemfuatia Kagere katika kufumania nyavu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ni John Bocco ambaye amefunga mabao matatu huku Emmanuel Okwi yeye akiwa amefumania nyavu mara mbili.

Mbali ya washambuliaji hao watatu, wengine walioifungia Simba mabao ni kiungo mshambuliaji Cletous Chama ambaye amefumania nyavu mara nne huku bao moja likiwa limefungwa na kiungo mkabaji, Jonas Mkude.

Habari zaidi soma Uk. 13 na 17.

Advertisement