Taifa Stars yailaza Equatorial Guinea, yakoleza safari ya Afcon 2021

BAO la la dakika za usiku lililofungwa na Abubakar Salum 'Sure Boy' limeiwezesha Taifa Stars kuvuna alama tatu katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Afcon 2021 baada ya kuifunga Guinea ya Ikweta mabao 2-1.
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Taifa ulishuhudiwa  Stars wakiutawala kwa asilimia kubwa lakini iliweza kujikuta ikienda mapumziko ikiwa nyuma bao 1-0.
Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa wenyeji kuutawala kutokana na mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa na nahodha wa  Stars, Mbwana Samatta aliyekuwa akisaidiana na Simon Msuva kuliandama lango la wapinzani.
Samatta alikosa kuiandikia bao Stars dakika ya pili baada ya mpira wake kuokolewa na Mlinda mlango wa Felipe Ovono ambaye alionesha umahiri wake wa kuokoa michomo.
Wakati vijana hao wa Kocha, Etienne Ndayiragije wakiendelea kulisakata soka mbele ya watazamaji waliojitokeza kwa wingi kutoa sapoti, walijikuta wakiruhusu bao dakika ya 15 lililofungwa na Petro Obiang ambalo lilidumu hadi mapumziko.
Hata hivyo Samatta alikosa nafasi nyingne ya kuisawazishia Stars dakika ya 40 lakini, Ovono aliweza kuzuia hatari hiyo langoni mwake na kuonekana kuwa kwenye ubora katika mchezo huo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Stars, kumtoa Hassan Kessy na nafasi yake kuchukuliwa na Ditram Nchimbi mabadiliko ambayo yalimfanya, Samatta kuwa huru katika uchezaji wake na yalifanikiwa kusawazisha bao.
Bao la Stars lilifungwa na  Simon Msuva dakika 68 baada ya kumzidi ujanja kipa wa Guinea ambaye muda mwingi alionekana kuwa kinara wa kuizuia Stars kufunga na hadi dakika za nyongeza, Sure Boy alipoachia shuti kali lililozama nyavuni na kuipa ushindi Stars mabao 2-1.
Kikosi kilichanza cha Stars kilikuwa na Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Kelvin Yonda, Hassan Kessy, Bakari Mwamnyeto, Salum Abubakar, Mbwana Samatta, Simon Msuva, Mohamed Hussein, Farid Mussa na Mzamiru Yassin.