Tanzania yajiweka pazuri tenisi Afrika

Dar es Salaam. Timu ya wasichana wa umri chini ya miaka 14 wa Tanzania, imeifunga Comoro katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yanayoendelea kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Tanzania ilianza kuvuna pointi baada ya kuifunga Comoro michezo yote mitatu na wavulana walishinda mchezo mmoja kati ya mitatu kwa umri chini ya miaka 16 dhidi ya Uganda.

Nasha Singo alifungua dimba kwa kumchapa Nayra Moustafa wa Comoro seti 2-0 za 6-1 na 6-1, Naitoti Singo alimchapa Rania Said kwenye singles seti 2-0 za 6-0 na 6-0 wakati katika mechi ya doubles, Nasha na Rachel waliwafunga Rania na Moinafatma kwa seti 2-0 za 6-0 na 6-0.

Kwa wavulana, Ismail Rashid alifungwa na Nsubuga Akram wa Uganda seti 2-0 za 6-4 na 6-3 wakati Kanuti Alagwa alimfunga Ocean Godfrey kwa seti 2-0 za 6-4 na 6-3. Kanuti na Ismail walipoteza katika doubles dhidi ya Ocen na Trevor kwa seti 2-0 za 7-6 na 6-1.

Matokeo hayo yameipa Tanzania pointi moja katika kundi la wasichana wa umri wa miaka 14 na wavulana wa miaka 16 walipunguzwa makali na Uganda wakati kwa wasichana wa miaka 16 Tanzania ilipoteza dhidi ya Kenya.

Roselinda Asumwa alimfunga Barbara Mollel kwa seti 2-0 za 6-1 na 6-0 na Alicia Owegi alimfunga Aurelia Mushi kwa seti 2-0 za 6-0 na 6-0 na katika doubles Watanzania hao walifungwa kwa seti 2-0 za 6-0 na 6-0.

Kwa wavulana chini ya miaka 14, Tanzania iliruhusu kipigo katika mechi zote tatu dhidi ya Burundi.

Aboubakar Malick alimfunga Isaka Ndossi seti 2-0 za 6-1 na 6-4, Allan Gatoto alimchapa Rashid Ramadhani kwa seti 2-0 za 7-5 na 6-1 wakati Gatoto na Mike waliwachapa Ndossi na Hassan katika Doubles kwa seti 2-0 za 6-1 na 6-3.

Mashindano hayo yatafikia tamati kesho na nchi itakayoshinda michezo mingi itatangazwa bingwa. Awali Alagwa alitwaa dhahabu, Rashid (fedha) na Naitoti (shaba) katika mashindano ya mkondo wa kwanza yaliyotoa pointi kwa mchezaji.