Tiboroha ajinadi akimtaja Manji Yanga

IMEFICHUKA kuwa kilichomsukua Jonas Tiboroha kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa Yanga SC ni hali mbaya kiuchumi iliyopo kwenye klabu hiyo kwa miaka miwili sasa.

Toboroha alisema  tangu alipojiuzulu Yusuf Manji,  viongozi wa Yanga wamekuwa kwenye sintofahamu na wengine kuamua kufuata nyayo zake na kuacha ombwe la uongozi kwenye klabu hiyo.

 "Baada ya viongozi wengi wa klabu yetu kujiuzuru,  klabu imeyumba sana katika kufanya mambo yake.

Viashiria vya klabu kuwa na  ombwe katika uongozi na kuyumba ni wachezaji na wafanyakazi kushindwa kupata mishahara na stahiki zao kwa wakati, " alisema.

Tiboroha alisema viashiria hivyo ndivyo vilivyomsukuma kuchukua fomu kugombea ili walau na timu yake waunganishe nguvu zao na wachama wa Yanga katika kuinusuru na kuisaidia klabu hiyo.

Wakati huohuo, Tiboroha  alimtaja aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji kuwa ndiye atakayekuwa mwanachama wa kwanza kumuomba awe muwekezaji katika klabu hiyo kutokana na kuwa na mawasiliano naye ya karibu.

"Kumekuwa na upotoshwaji usiokuwa na tija kwa klabu kwamba mimi nina ugomvi na Manji sio kweli mara ya mwisho kufanya mazungumzo naye ni mwezi uliopita na natambua umuhimu wake katika klabu hii nitazungumza nae ili aweze kuwekeza," alisema.