Tshabalala asaini Msimbazi, usajili Simba, Yanga gumzo

Muktasari:

Simba na Yanga zimeingia sokoni kuwania saini za wachezaji hasa wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha timu zao.

Dar es Salaam. Beki wa Mohamed Hussen ‘Tshabalala’ ameongeza mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba ukiwa ni mwendelezo wa mabingwa hao na watani zao Yanga kujenga vikosi vyao kwa ajili ya mashidano ya kimataifa msimu ujao, umewaibua makocha wakongwe nchini.

Wakati Simba na Yanga zitacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC na KMC zitacheza Kombe la Shirikisho. Michuano ya kimataifa msimu huu imepangwa kuanza Agosti 9, mwaka huu.

Simba na Yanga zimeingia sokoni kuwania saini za wachezaji hasa wa kigeni kwa ajili ya kuimarisha timu zao.

Yanga imesajili wachezaji saba wa kigeni ambao ni mabeki, Lamine Moro (Ghana) na Mustapha Selemani (Burundi). Washambuliaji, Sadney Ukhob (Benin), Issa Bigirimana (Burundi), Patrick Sibomana (Rwanda), Juma Balinya (Uganda) na Kalengo Maybin (Zambia).

Wachezaji wazawa ambao tayari Yanga imethibitisha kuwasajili ni kiungo Mzanzibar, Abdulaziz Makame, beki Ally Ally na Mapinduzi Balama anayecheza nafasi ya kiungo.

Simba kwa upande wake imemsajili beki Msudani Shiboub Sharafeldin na mshambuliaji Wilker Henrique Da Silva kutoka Brazil ambao wale wa zamani Meddie Kagere (Rwanda), Pascal Wawa (Ivory Coast) na Clatous Chama kutoka Zambia.

Pia Simba imemsajili kipa Beno Kakolanya, Miraji Athumani na beki wa kati, Kennedy Wilson.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Kocha wa Tanzania Prisons, Mohammed Rishard ‘Adolf alisema usajili wa Simba na Yanga una maana kubwa kwa miamba hiyo ya soka nchini.

“Hatuwezi kueleza ubora wa mchezaji mmoja mmoja hadi wacheze tuwaone, lakini naamini kwa kipindi hiki kila klabu inapambana kufanya usajili bora kuongeza nyota wa kigeni ambao wataibeba timu,” alisema Rishard.

Alisema hiki ni kipindi cha wachezaji wazawa kutobweteka na kuwapa fursa wale wa kigeni ambao wanaweza kuchukua nafasi zao katika kikosi cha kwanza.

Alisema wingi wa wachezaji wa kigeni wanaosajiliwa na Simba na Yanga haupaswi kupuuzwa kwa kuwa wanaweza kuwapoka nafasi zao na kuua vipaji vyao.

Kocha Kenny Mwaisabula alisema anaamini usajili wa Simba na Yanga unafanywa kutokana na upungufu ulioonekana msimu uliopita una lengo la kuziba mapengo.

“Ni usajili unaotoa imani kwa pande zote mbili, tuwasubiri tuone uwanjani, lakini naamini si Simba wala Yanga ambaye kipindi hiki atakubali kuona mwenzake anang’ara kimataifa wakati yeye anapotea.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema usajili wa klabu hizo una malengo na unafanyika kiufundi kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi.

“Kikubwa ni maandalizi kwasababu mpira unachezwa uwanjani, kila moja inasajili kwa malengo ya timu na nini wanahitaji hivyo tusubiri tuone,” alisema Kibadeni.