LIGI KUU: Umbali tishio ubingwa Simba

Dar es Salaam. Wakati Simba leo ikishuka dimbani kuvaana na Alliance, timu hiyo inakabiliwa na kibarua kigumu cha kumaliza mechi zake 14 zikiwemo za viporo kutokana na umbali mrefu itakaokabiliana nao.

Simba ina mtihani mgumu wa kupata matokeo mazuri katika mechi zake kutokana na ukaribu wa mechi moja hadi nyingine.

Ratiba inaonyesha Simba itacheza mechi zake kwa tofauti ya siku mbili au tatu huku baadhi ya mikoa mingine italazimika kutumia usafiri wa basi.

Simba inalazimika kucheza mechi zake karibu kwa kuwa ilikuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo katika mechi ya robo fainali.

Timu hiyo leo itacheza na Alliance baada ya kumalizana na Kagera Sugar kabla ya kuivaa KMC wiki hii. Mechi zote mbili zitachezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Simba ilisafiri umbali wa kilometa 416 kwenda Mwanza ikitokea mkoani Kagera kupepetana na Alliance.

Aprili 26 itacheza na KMC kabla ya kusafiri kilometa 218 kwenda Mara kuvaana na Biashara United Aprili 28.

Biashara United na Simba zitacheza mechi ya kiporo ya mzunguko wa kwanza kabla ya kurudiana Dar es Salaam.

Simba itasafiri kwenda Dar es Salaam sawa na kilometa 1370 na Aprili 30 itakuwa Uwanja wa Taifa kumenyana na JKT Tanzania.

Pia Simba itasafiri umbali wa kilometa 822 kwenda Mbeya na Mei 3 itacheza na Mbeya City ambapo siku tatu baadaye Mei 6 itavaana na Prisons kwenye uwanja huo.

Mei 7 Simba itasafiri kwenda Dar es Salaam sawa na kilometa 822 na Mei 8 itaivaa Coastal Union Uwanja wa Taifa.

Ratiba inaonyesha Mei 10 itacheza na Kagera Sugar kabla ya Mei 13 kupepetana na Azam, Mei 16 itacheza na Mtibwa Sugar na baadaye Mei 19 dhidi ya Ndanda.

Mei 20, Simba itasafiri kwenda Singida sawa na kilometa 696 na Mei 22 itakuwa Uwanja wa Namfua kucheza na Singida United. Mei 23 itarejea Dar es Salaam sawa na kilometa 696 kuikabili Biashara United.

Mei 26 itakwenda Morogoro sawa na kilometa 192 na Mei 28 itacheza mechi ya mwisho ya kumaliza msimu huu dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kauli ya Kocha

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema ratiba inatakiwa kuangaliwa upya kwa kuwa itawabana kucheza mechi kila baada ya siku mbili na inaweza kuhatarisha afya za wachezaji wake kabla ya kumalizika kwa mashindano. “Naona kila mechi itakuwa ngumu kulingana na ratiba, lakini nitakuwa nafanya mabadiliko ili kumpa nafasi kila mchezaji na wengine kupumzika ili kuendelea kuwa na ari ya ushindani na kupata pointi tatu katika kila mechi,” alisema Aussems.

Tshabalala

Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema wachezaji watakuwa na kazi ngumu ya kushindana tofauti na mechi zao za awali kwenye mashindano hayo. “Hakuna namna ratiba imeshapangwa wachezaji tutapambana na kushindana kwa hali yoyote ile, hii ndio kazi yetu tunalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu na mepesi,” alisema Tshabalala.

Mayay

Mchambuzi wa soka Ally Mayay alisema makosa yalifanyika Simba ilipokuwa katika mashindano ya kimataifa ingawa ilikuwa na muda wa kupunguza mechi za viporo. “Wachezaji wao watachoka kwa sababu watasafiri umbali mrefu, hawatakuwa na muda wa kutosha kupumzika na kufanya mazoezi kwa maana hiyo naona mechi zao zitakuwa ngumu zote na kama wasipokuwa makini wanaweza kujikuta katika wakati mgumu kupata pointi tatu,” alisema Mayay.

Daktari

Daktari wa mifupa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) Paul Mareale, alisema kitaalamu klabu zinatakiwa kuwa na wataalamu wa kuwafanyia wachezaji mrejesho wa kiafya (recovering) ili kurudisha hali zao za misuli na mifupa ili kutoa fursa ya kushindana katika mechi nyingi.

“Kiafya muda mwingine ni bora mchezaji kucheza mara kwa mara kwani anakuwa katika hali ya ushindani kama wenzatu Ulaya wanavyofanya

“Lakini miondombinu ya kusafiri huwa ndio tatizo, lakini njia nyingine kwa Simba kulikabili hilo ni kufanya mabadiliko katika matumizi ya wachezaji ndio maana walisajili 27,” alisema Mareale ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).