Ushuhuda wangu kwa Mbwana Samatta (1)

Muktasari:

  • Kuanzia African Lyon ndipo nilipomuona Samatta. Kando yake alicheza sambamba na fundi mwingine, Yusuf Soka. Ilionekana Soka alikuwa staa kuliko Samatta nyakati zile. Alikuwapo pia fundi mwingine wa mpira, Rashid Gumbo. Baadaye pia alikuja Robert Ssentongo kutoka Uganda.

NILIJUA Mbwana Samatta angefika mbali zamani. Kwa mara ya kwanza jina lake lilikatisha kwangu kupitia katika namba moja ya msomaji wa makala zangu miaka mingi iliyopita. Mpaka leo sijawahi kukutana na msomaji yule. Hadi leo sijui alipo.

Ningependa siku moja huyu msomaji ajitokeze na kuniambia kwamba ni yeye ndiye aliyeniandikia meseji ile kuhusu ubora wa Samatta. Wakati ule nilikuwa naacha namba yangu ya simu chini ya kila kolamu yangu ya HISIA ZANGU.

Msomaji aliandika ‘Bro Edo achana na hao washambuliaji wenu hapo uwanja wa Taifa. Huku Mbagala kuna mtoto anacheza Mbagala Market anajua sana aisee. Anaitwa Mbwana Samatta. Ana kila kitu. Anafunga sana. Kila siku anafunga mabao manne, mara matano.”

Aliandika kitu kama hicho. Jina lilinikaa kichwani. Mbwana Samatta. Wakati huo alikuwa akicheza Mbagala Market. Sikuwahi kumuona. Siku moja nikasikia amefunga mabao saba katika mechi moja. Bado sikuwahi kumuona.

Baadaye akatua klabu ya African Lyon ambayo wakati huo ilikuwa inamilikiwa na tajiri, Mohamed Dewji. Kwa sasa Mo na Samatta wote ni matajiri. Wakati huo alikuwa mtoto fulani tu asiye na hadhi kubwa kule Mbagala.

Kuanzia African Lyon ndipo nilipomuona Samatta. Kando yake alicheza sambamba na fundi mwingine, Yusuf Soka. Ilionekana Soka alikuwa staa kuliko Samatta nyakati zile. Alikuwapo pia fundi mwingine wa mpira, Rashid Gumbo. Baadaye pia alikuja Robert Ssentongo kutoka Uganda.

Pale ndipo niliposhuhudia kipaji cha Samatta. Zaidi ya kila kitu alichokuwa nacho, binafsi nilipenda uwezo wake wa kujiamini. Wachezaji wa Tanzania, wale wenye vipaji na wale wasio na vipaji, wote wana tatizo moja. Papara. Samatta hakuonekana kuwa mmoja wao.

Baada ya African Lyon kuvurugwa na Mo kukata tamaa, Samatta alichukuliwa na Simba. Siku za kwanza hakwenda kuripoti Simba. Nasikia kuna wenzake kule kwao Mbagala walikuwa wanamtisha kwamba Simba kulikuwa na ushirikina mkubwa.

Lakini kilichojulikana kwa wengi ni kwamba Simba ilikuwa imemuahidi Samatta gari aina ya Toyota Chaser na hawakumtimizia. Ilikuwa mwaka 2010 hiyo. Toyota Chaser ilikuwa moja kati ya magari ya Kijapan yenye hadhi mkubwa nchini hapa.

Haikueleweka kwamba Samatta alikuwa anakimbia ushirikiana, au alikuwa ameweka msimamo wake wa kupewa gari. Wakati huo Simba ilikuwa inasuasua kwa muda mrefu katika safu yake ya ushambuliaji. Sawa, Mussa Hassan Mgosi na Emmanuel Okwi walikuwa mastaa lakini Simba ilijua kwamba ilikuwa inamuhitaji Samatta.

Baada ya kutimiziwa alichotaka, hatimaye Samatta aliripoti kambi ya Simba baada ya kukosekana kwa takribani miezi mitatu. Alipoingia tu kikosini Samatta alionyesha ubora wa hali ya juu na kutishia kwa kiasi kikubwa nafasi ya staa mkubwa klabuni, Mgosi.

Samatta alikupa kila kitu unachotaka. Chenga, mashuti wakati akiwa katika mwendo, mabao ya miguu yote, mabao ya hewani, pasi za mwisho na uwezo mkubwa wa kujiamini. Alifunga kwa namna alivyojisikia.

Alifanya mambo makubwa Simba na kabla hata hawajacheza na TP Mazembe pale uwanja mkubwa wa Taifa, tayari safari ya Samatta ilianza kuonyesha dalili katika pambano dhidi ya Mtibwa Sugar pale Shamba la Bibi.

Kabla ya mechi nilimnyanyua ofisini mwandishi mkongwe wa habari za michezo, Samson Mfalila akamtazame mchezaji ambaye nilimwambia ana uwezo wa kucheza soka Ulaya. Mbwana Samatta. Mfalila alikuwa anamsikia tu Samatta lakini hakuwahi kumuona.

Samatta alimkaribisha Mfalila katika ulimwengu wake wa soka kwa kupiga kitu ambacho Waingereza wanaita ‘perfect hat trick’. Alifunga mabao matatu - moja akitumia kichwa, moja mguu wa kushoto, na jingine mguu wa kulia. Bao alilofunga kwa kutumia mguu wa kulia linabakia kuwa moja kati ya mabao bora Zaidi kuwahi kufungwa katika historia ya uwanja wa Shamba la bibi.

Samatta aliutuliza mpira katikati ya uwanja akamfuata mchezaji mmoja wa Mtibwa akampiga chenga, halafu akampita wa pili, halafu wa tatu, halafu wa nne, kisha akapiga shuti kali lililokwenda katika nyavu za Mtibwa. Shuti alipiga akiwa nje ya kumi na nane ya Mtibwa.

Kasi yake huku akiwa anamiliki mpira ilikuwa kubwa. Kwa wenye kumbukumbu nzuri, bao hili halikutofautiana sana na bao ambalo Diego Maradona, akiwa katika jezi ya Argentina, aliwafunga Waingereza pale Mexico mwaka 1986.

Tofauti ni kwamba Maradona alimlamba chenga golikipa. Samatta hakumlamba ila aliamua kupiga shuti kali la mbali. Safari ya Mbwana ilianzia pale. Alifanya mambo ya kujiamini kupita kiasi. Wakati anaondoka uwanjani mashabiki wote walimtazama kwa jicho la husuda akiondoka na mpira wake. Hata lilipowadia pambano dhidi ya Mazembe ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya Samatta kujitangaza kimataifa. Ni mashabiki wa Mazembe ndio walimwambia tajiri wao, Moise Katumbi kwamba lazima waondoke na Samatta.

Mechi mbili za Samatta dhidi ya Mazembe zilimpeleka Lubumbashi kwa uhamisho kwa dola 100,000. Wakati ule ulikuwa uhamisho wa kwanza wa mchezaji wa Kitanzania uliostaajabisha sana. Dola laki moja!. Haikuwahi kutokea. Leo Samatta ameuzwa pahala kwa Pauni 10 milioni (takriban Sh.30 bilioni). Nyakati zinakwenda kasi.

Kama tulivyomsubiria Samatta kufunga bao lake la kwanza Genk, kama tunavyomsubiria Samatta kufunga bao lake la kwanza Aston Villa, basi ndivyo tulivyomsubiria Samatta kufunga bao lake la kwanza Mazembe. Tukatega sikio.

Tukaanza kusikia. Mara leo kafunga moja, kesho hat trick, keshokutwa angefunga mawili. Baadaye angefunga moja. Kelele zikaanza kusikika kuhusu ufalme wa Samatta kule Lubumbashi. Baadaye tukaanza kusikia kuhusu ufalme wa Samatta Congo. Ni katika nyakati hizo pia, Thomas Ulimwengu alitua Mazembe.

Ilionekana Mfalme namba moja alikuwa Tresor Mputu, halafu Samatta alikuwa anaunyatia ufalme huo kwa kasi licha ya kuwepo kwa mastaa wengine wa Congo na Zambia ndani ya kikosi cha Mazembe. Walikuwepo kina Andrew Sinkala, Reinford Kalaba, Stopilla Sunzu, Patchou Kabangu na wengineo.

Sikutaka kupitwa. Agosti, 2012 nilikuwa mwandishi wa kwanza kutoka Tanzania kusafiri kwenda Lubumbashi kwa ajili ya kufanya mahojiano na Samatta. Wa kwanza kabisa. Nilitaka kwenda kujionea ufalme wa Samatta kwa macho yangu. Itaendelea kesho Jumapili