VIDEO: Eymael awashanga mashabiki wa Yanga kumshangilia Morrison

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga SC, Luc Eymael amesema hakuvutiwa na kitendo alichofanya mshambuliaji wake Benard Morrison cha kutembea juu ya mpira katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Tanzania Prisons.

Kocha huyo, Mbelgiji alisema Morrison aliwakosea heshima wapinzani wao, ambao katika mchezo huo, alifunga bao kwa mkwaju wa penalti na kutengeneza la pili lililofungwa na Yikpe Garmien, wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.

"Alicheza vizuri sana, lakini sikuvutiwa hata kidogo na kitendo alichokifanya cha kuwakosea heshima wapinzani wetu, nilishangaa kuona mashabiki wakimshangilia, ni upuuzi ule, sikuvutiwa nao na nilimweleza hilo," alisema kocha huyo.

Eymael alisema huwezi kukuta washambuliaji wakubwa dunia kama Sadio Mane wa Liverpool akifanya upuuzi ule hata kama klabu yake au taifa lake analolichezea likiwa linaongoza kwa utofauti mkubwa wa mabao.

Mechi ya Kombe la Shikirisho la Azam dhidi ya Tanzania Prisons, ilikuwa ni wa pili kwa Morrison kuichezea Yanga, wa kwanza ulikuwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Singida United.

Katika mchezo wake wa kwanza, alitengeneza mabao mawili ya Yanga huku akitembea juu ya mpira kama alivyofanya katika mchezo wake wa pili dhidi ya Prisons.

Kocha Eymael amevutiwa na namna ambavyo kikosi chake kimekuwa kikiimarika kwa kusema,"Nataka kuona tukicheza soka la kuvutia na kupata matokeo kama ilivyokuwa katika michezo miwili iliyopita."

Eymael hakuwa na mwanzo mzuri katika kikosi cha Yanga kutokana na kupoteza michezo miwili mfululizo ambayo ni dhidi ya Kagera Sugar na Azam.