Wadau watofautiana kipigo Simba

Dar es Salaam. Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha wa Simba, Patrick Aussems katika mchezo wa robo fainali dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo yameonekana kuibua mjadala.

Baadhi ya wadau nchini wametoa maoni kuhusu mabadiliko aliyofanya Aussems kwa kuwatoa Juuko Murshid, Mzamiru Yassin na kumuanzisha benchi Meddie Kagere katika benchi.

Pia alimtoa Emmanuel Okwi na nafasi yake kujazwa na mshambuliaji kinda Rashid Juma. Katika mchezo huo, Simba ilichapwa mabao 4-1.

Kitendo cha Aussems kumtoa Juuko anayecheza nafasi ya beki wa kati akichukua nafasi ya majeruhi Pascal Wawa, kilionekana kuyumbusha ngome ya Simba katika mchezo huo.

Hesabu za Aussems kumuingiza Clatous Chama kujaza nafasi ya Mzamiru na Kagere kumrithi Juuko ziligonga ukuta kwani eneo la kiungo lilipwaya na kutoa nafasi kwa TP Mazembe kutawala eneo la katikati.

Chama alishindwa kutoa msaada timu ilipokuwa ikishambuliwa baada ya mchezaji mwingine wa kiungo James Kotei kuzidiwa maarifa na wachezaji wa katikati wa TP Mazembe.

Kitendo cha safu ya kiungo kupwaya, kilitoa fursa kwa TP Mazembe kumiliki eneo la katikati na kutumia zaidi mipira ya pembeni hasa kwa beki Zana Coulibaly.

Wakati Aussems akifanya mabadiliko hayo Simba ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1 dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Aussems alonga

Akizungumza jana, Aussems alisema hawezi kuzungumzia mabadiliko aliyofanya kwa kuwa ni masuala ya kiufundi.

“Siwezi kuzungumzia mabadiliko niliyofanya kwa sababu ni mambo ya kiufundi,” alisema kocha huyo kwa kifupi.

Hata hivyo, Aussems alisema TP Mazembe ni timu imara yenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa.

Kauli ya Pazi, Msolla

Akizungumzia mabadiliko aliyofanya Aussems, kipa nguli wa zamani wa Simba, Idd Pazi alisema kocha huyo alifanya kosa kumtoa Juuko ambaye alikuwa mhimili katika nafasi ya ulinzi.

“Juuko ndiye alikuwa amebaki nyuma baada ya Wawa (Pascal) kuumia, unamtoa unamuingiza fowadi ili akabe au,” alihoji Pazi.

Kocha huyo wa makipa alisema Simba ilipaswa kutulia baada ya wapinzani wao kupata bao la kusawazisha, lakini badala yake wachezaji walipotea na kuchangia kuongezwa bao la pili.

Wakati Pazi akitoa kauli ya kukosoa mabadiliko ya Aussems, mchambuzi wa soka na nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema TP Mazembe ilikuwa na nafasi ya kushinda mchezo huo.

“Hakuna sababu ya kumlaumu kocha, angalieni na ubora wa Mazembe ilimiliki mpira kwa asilimia 70, isitoshe Simba ilikuwa imeshafungwa, kocha alikuwa anajaribu ili kuona kama wachezaji anaoingiza watabadili matokeo, lakini ilishindikana,” alisema Mayay.

Mayay alisema Simba imefanya kazi kubwa na inastahili pongezi kwa kufika tu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msolla ambaye ni kocha wa zamani wa Taifa Stars, alisema mbinu aliyotumia Aussems kumuanzishia benchi Kagere imekuwa ikitumiwa na makocha wengi akiwemo yeye.

“Mashabiki wasimlaumu kocha kumuanzisha benchi Kagere inawezekana lengo lake lilikuwa ni kumpa nafasi ya mchezaji kusoma mchezo ili kuleta mabadiliko chanya.

Hata hivyo, Msolla alisema Simba ina tatizo katika matumizi ya viungo na mabeki aliodai kuwa wamekuwa wakifanya makosa yanayojirudia.