Wakili akana Ronaldinho kutumia paspoti feki

Muktasari:

  • Nyota huyo wa zamani wa Barcelona na AC Milan alikamatwa Jumatano kwa tuhuma kuwa alitumia hati za kughushi za kusafiria kuingia Paraguay.

Mwanasheria wa nyota wa zamani wa soka wa Brazil, Ronaldinho amekanusha tuhuma kuwa kiungo huyo na kaka yake walitumia hati za kughushi za kusafiria kuingia nchini Paraguay.
Nyota huyo aliyetwaa Kombe la Dunia na kaka yake walihojiwa kwa zaidi ya saa saba na waendesha mashtaka wa serikali kutokana na tuhuma kuwa waliingia Paraguay kwa kutumia paspoti zilizoghushiwa.
Ronaldinho alikuwa amealikwa katika mji mkuu wa Paraguay na taasisi inayojihusisha na watoto wenye mahitaji, na pia kutangaza kitabu kipya.
Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 39 na kaka yake walienda ofisi ya mashtaka jana asubuhi pamoja na mwanasheria wao, Adolfo Mari Alhamisi kujibu tuhuma kuwa walitumia hati hizo za kughushi kuingia Paraguay.
"Waliamua kwa hiari yao kutoondoka na kujipeleka kwa mwendesha mashtaka wa serikali," alisema Marin.
Ronaldinho "hakuhitaji kutumia hati nyingine yoyote zaidi ya halisi aliyonayo," alisema Marin.
Kwa mujibu wa ofisa anayeongoza uchunguzi, Gilberto Fleitas, nyota huyo wa zamani alipewa hati ya kughushi na mfanyabiashara wa Brazil, Wilmondes Sousa Lira, ambaye amekamatwa.
Marin alisema Ronaldinho alimwambia mwendesha mashtaka wa serikali kuwa hati aliyonayo alipewa nchini Brazil mwezi mmoja uliopita.
Ronaldinho, ambaye amewahi kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mara mbili, na kaka yake walikamatwa Jumatano wakiwa hotelini.
Hati zao ziling'amuliwa wakati walipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Asuncion, kwa mujibu wa mwendesha mashtaka kiongozi, Federico Delfino.
Nyota huyo wa zamani wa klabu za Barcelona, AC Milan na Paris Saint-Germain na kaka yake walisafiri kwa kutumia "paspoti zilizoghushiwa na vitambulisho feki," alisema Delfino.
Mamlaka nchini Brazil zilimpokonya Ronaldinho hati ya kusafiria mwezi Novemba, 2018 baada ya kushindwa kulipa faini ya dola 2.5 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh5 bilioni za Kitanzania) kutokana na kuharibu mazingira wakati akijenga nyumba yake.