Wawa, Yondani, Kanda, Molinga wabadilisha upepo ghafla Yanga, Simba

Tuesday March 24 2020

 

By CHARLES ABEL

UNAWEZA usiamini, lakini ndio ukweli ulivyo kwamba maisha ya nyota nane wa Simba na Yanga yamebadilika ghafla ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili tofauti na kile kilichotegemewa.
Ndio, imekuwa kama utani vile, kwanza walionekana si mali kitu kisha ghafla tu wamegeuka kuwa lulu na kufurahia maisha ndani ya klabu hizo kubwa nchini.
Ni hivi. Baadhi ya nyota waliokuwa katika wakati mgumu na uwezekano wa kutupiwa virago mwishoni mwa msimu, wamegeuka kuwa lulu na kujiweka katika mazingira mazuri ya kuendelea kubakia katika timu hizo na kuvuna kiasi kikubwa cha fedha za usajili.
Kadhalika wengine wamejikuta wakiporomoka ghafla na kupoteza nafasi zao kwenye vikosi vya timu hizo na huenda wakatemwa mara baada ya msimu huu kumalizika.

WAWA, DEO KANDA
Katika kundi la wachezaji hao nane, wanne ambao ndani ya muda mfupi wamebadilisha hali ya hewa kutoka kufikiriwa kutemwa hadi kuwa na uhakika wa kubaki na kuongezewa mikataba ni Deo Kanda na Pascal Wawa upande wa Simba, Jaffari Mohamed na Said Juma ‘Makapu’ katika kikosi cha Yanga.
Wawa amekuwa roho ya safu ya ulinzi ya Simba kutokana na uwezo wake wa kukabiliana na washambuliaji wa timu pinzani lakini pia kuichezesha timu kutoka nyuma jambo ambalo limefanya awe kipenzi cha kocha Sven Vandenbroeck.
Kabla ya msimu huu kuanza, beki huyo aliigawa Simba ambapo wapo waliotamani abakie na kuna waliopendekeza aachwe na baadaye akaongezewa mkataba wa mwaka mmoja kwa hesabu za kuachwa mwishoni mwa msimu lakini sasa amekuwa miongoni mwa nyota watakaobakia kwa kuongezewa mikataba kwa pendekezo la benchi la ufundi.
Ukiondoa Wawa, kuna Deo Kanda ambaye mwanzoni hakuwa na namba ya kudumu kutokana na majeraha na pia benchi la ufundi kutompa nafasi lakini sasa amekuwa lulu.
Winga huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na kufunga, hakuonekana kama angeweza kubakia klabuni baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika, ila taarifa za uhakika zilizopo ni kwamba Simba inajipanga kumalizana na TP Mazembe inayommiliki ili imsajili jumla.

MAKAPU. JAFFAR WAMO
Ukiondoa wawili hao, ndani ya kikosi cha Yanga kuna Said Juma ‘Makapu’ na Jaffar Mohammed ambao maisha yamewanyookea ghafla licha ya kuwa katika hali tete miezi michache iliyopita.
Makapu anayemudu kucheza vyema nafasi za ulinzi na kiungo, ilikuwa atemwe na Yanga baada ya msimu uliopita kumalizika kutokana na kiwango chake kuonekana hakikuridhisha benchi la ufundi lakini sasa amekuwa lulu ndani ya timu hiyo.
Tangu ujio wa kocha Luc Eymael Januari, Makapu amekuwa na namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza na ni wazi kwamba ataongezwa mkataba mpya ingawa mwanzoni hakuonekana kuwa mchezaji muhimu kikosini.
Pia kuna kiungo kiraka, Jaffar naye ni kama ameokolewa na ujio wa Eymael, kwani awali alikuwa anasugua benchi na usajili wake ulionekana kama umefanyika baada ya Yanga kuwakosa wachezaji  waliokuwa kipaumbele chao ila kwa sasa ndiye kipenzi cha kocha katika nafasi ya beki wa kushoto akimpiku Adeyum Ahmed aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili.

YONDANI, SHIBOUB MTEGONI
Wakati hali ikiwa hivyo kwa nyota hao, wenzao wanne wamejikuta kikaangoni na wapo katika uwezekano mkubwa wa kutemwa licha ya kuanza vizuri ndani ya timu hizo.
Mkongwe Kelvin Yondani licha ya kuanza na kucheza sehemu kubwa ya msimu huu akiwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Yanga, amepoteza namba ghafla chini ya Eymael ambaye amependekeza nyota huyo aachwe mwishoni mwa msimu.
Ukiondoa Yondani, mwingine ndani ya Yanga anayeweza kupewa mkono wa kwaheri licha ya kuanza vizuri ni kiungo Abdulaziz Makame ambaye tangu alipokuja kocha Eymael, amekuwa akisotea benchi.
Kwa upande wa Simba, kiungo Sharaf Shiboub ambaye alianza vizuri msimu, sasa hana nafasi kikosini na ni wazi kwamba atatemwa mwishoni mwa msimu baada ya kushindwa kuhimili ushindani wa namba kwa viungo kwenye timu hiyo.
Ukiondoa Shiboub, beki wa kushoto Gadiel Michael licha ya kusajiliwa kibabe akionekana anakwenda kuchukua nafasi mbele ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kwa sasa hana namba na majaliwa yake kwenye timu hiyo yako shakani.

SIKIA WADAU SASA
Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema kinachowaangusha na kuwabeba wachezaji hao ni nidhamu.
“Shida kubwa ya wachezaji wengi ni kukosa nidhamu. Wakishaona wanapata nafasi wanaanza kukosa nidhamu na kutozingatia wajibu wao sasa makocha wa kizungu siku zote huwa hawana mambo ya kupenda mtu.
Hao wanaofanya vyema sasa ni wale ambao nidhamu yao ipo juu na wanafanya kile wanachoelekezwa. Na makocha wa kizungu wakishakoshwa na kiwango cha mchezaji mara moja tu ni vigumu kwa mchezaji huyo kukaa benchi tena,” alisema Julio.
Kocha Felix Minziro alisema sababu inayopelekea hilo ni kujitambua na kutojitambua kwa wachezaji.
“Wachezaji wengi wanakosa misingi ya kiweledi. Wamekuwa wakiishi maisha ambayo mara kwa mara huhatarisha viwango vyao. Na huwa hawafikirii athari za kile wanachokifanya. Unaweza kukuta mchezaji anakutana na changamoto za nje ya uwanja, anaamua kutotimiza wajibu kwa kugomea mazoezi au kucheza chini ya kiwango pasipo kujua kwamba kwa hilo anajipoteza. Kiufupi tuna tatizo la kujitambua kwa wachezaji wetu,” alisema Minziro.

Advertisement