Yanga sasa yaweka rehani ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara

Friday January 19 2018

 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

 Baada ya kutoka suluhu na Mwadui, timu ya Yanga imezidisha presha ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Pia ubora wa kikosi hicho unatia shaka kama inaweza kushiriki kikamilifu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwezi ujao.

Yanga juzi ilicheza soka ya kiwango cha chini kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku safu ya ushambuliaji ikionekana kuwa butu.

Mbali na klabu hiyo kutikisika kiuchumi, lakini haijafanya usajili wa nguvu ambao utakuwa chachu ya kushindana vyema ndani na nje ya nchi.

Pia idadi kubwa ya wachezaji majeruhi, imetajwa kuwa moja ya sababu inayoipa Yanga kibarua cha kutwaa ubingwa au kutoa ushindani katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Udhaifu

Yanga imeshindwa kucheza soka ya ushindani inapocheza na timu yenye ngome imara au inayotumia mabeki watano nyuma wakiungana na kiungo mkabaji (namba sita).

Tatizo la Yanga lilijitokeza katika mchezo waliotoka sare ya bao 1-1 na Majimaji FC, kabla ya kupata ushindi mwembamba 1-0 dhidi ya Ndanda FC.

Pia kasoro hizo zilijitokeza na Lipuli FC, Prisons ya Mbeya na katika mchezo wa Kombe la FA ilipomenyana na Reha FC licha ya kushinda mabao 2-0.

Ubora wa safu ya ushambuliaji kwa Yanga ulijirudia dhidi ya Mwadui iliyotumia idadi kubwa ya mabeki na viungo kulinda lango.

“Niliwaambia wachezaji wangu kama tukishindwa kufunga tusifungwe ndivyo ilivyotokea, walicheza kwa usikivu kwa kufuata maelekezo,” alisema kocha wa Mwadui Ally Bizimungu.

Mkcha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ alisema ubutu wa safu yake ya ushambuliaji imechangiwa na idadi kubwa ya wachezaji majeruhi.

Pawasa, Mayay wapasua jipu

Beki kisiki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa alisema Yanga imeshindwa kutamba kwa kuwa inapitia kipindi kigumu.

“Yanga ipo kwenye kipindi cha mpito Chirwa amefungiwa, Ngoma majeruhi na Tambwe ambaye hivi karibuni alitokea katika maumivu hayuko fiti ukimuondoa mshambuliaji chipukizi Yohana Nkomola.

“Kama washambuliaji wote wakiwa kwenye kiwango kizuri makali ya Yanga kwenye eneo la ushambuliaji yatarejea,” alisema Pawasa.

Nahodha wa zamani wa Yanga Ally Mayay alisema timu hiyo imeshindwa kucheza kwa kiwango bora kutokana na tatizo linaloanzia katika eneo la kiungo mshambuliaji.

“Kipindi cha kati Yanga ilitulia baada ya kuwa na muunganiko mzuri wa Chirwa na Ajibu naona changamoto inamkabili kocha Lwandamina katika mashindano ya kimataifa,” alisema Mayay.     

Advertisement