Ulinzi wa kufa mtu tamasha la Fiesta Uwanja wa Uhuru

Muktasari:

  • Tamasha hili la Fiesta lilianza mwaka 1999, likitambulika kama Summer Jam na mwaka 2003, lilibadilika jina na kuitwa Fiesta hadi sasa

Dar es Salaam. Hali ya ulinzi imeimarishwa eneo la kuzunguka Uwanja wa Uhuru linapofanyika tamasha la Fiesta.

Eneo lote la Uwanja wa Uhuru na Taifa kuna gari kubwa la washawasha na gari dogo la Polisi wakizunguka kuhakikisha usalama unakuwa.

Katika mageti ya viwanja vyote viwili kuna askari wa Suma JKT wasiopungua nane kila geti.

Mbali ya askari wa Suma JKT kuna walinzi wa kampuni binafsi nje na ndani ya uwanja wanaozunguka kila kona ya uwanja.

Mpaka sasa hali ni shwari na mashabiki wanaendelea kuingia kwa utulivu.

Nje ya uwanja misululu ya mashabiki wanaokata tiketi ni mirefu. Huku upande wa Sh 5000 ikiwa na nafuu ukilinganisha na ile ya Sh 3000.

Mashabiki walianza kuingia uwanjani hapo saa 10:00 jioni, walikuwa wakiimba huku wakicheza nyimbo zilizokuwa zikisikika kwenye spika za uwanjani hapo.

 

Tamasha hili la Feista lilianza mwaka 1999, likitambulika kama Summer Jam na baadae ndio likaja kubadilika jina.

Mwaka 2003, ndio lilibadilika jina na kuitwa Fiesta na hii inakuwa mara ya 15, tangu kuanzishwa kwake.

Halikufanyiika mwaka 2015 kutokana na kuwapo kwa uchaguzi mkuu.

Katika hatua nyingine mambo ambayo yatakuwepo katika tamasha hili ni burudani ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali hapa nchini pamoja na burudani nyingine kama kula na kunywa.

Wasanii ambao watapanda katika jukwaa hili watakuwa zaidi ya 30, ila kati ya hao ni Rostam, Alli Kiba, Mr Blue, Harmonize, Juma Nature, Marioo na wengine wengi.

Tamasha inakuwa mara ya pili kufanyika uwanja wa taifa na itakuwa mara ya tatu kutokufanyika katika viwanja vya Leaders kama ambavyo imezoeleka katika miaka mingi iliyopita.