Mwenendo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini

Mwaka 2010 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya ifikapo mwaka 2030 watu 52 milioni duniani watafariki kutokana na magonjwa yatokanayo na mtindo wa maisha (NCDs).

Maradhi yasiyoambukiza ni kama kisukari, saratani, matatizo ya moyo na yanayoathiri mfumo wa upumuaji. Mengine ni figo na ini yanayozidi kuongezeka siku baada ya siku.

Ingawa Tanzania ilianza kampeni dhidi ya maradhi hayo miaka mitatu iliyopita, bado hakuna mafanikio makubwa kwa kuwa juhudi hizo zinategemea utayari wa watu kushiriki ili wapate taarifa za kujikinga.

Hata hivyo wataalamu waliozungumza na Mwananchi wameonya tabia za kila siku au mtindo wa maisha kuwa chanzo cha magonjwa mengi yasiyoambukiza.

Wataalamu wa afya wanathibitisha kuwa aina ya vyakula ni chanzo cha baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza na kwa mujibu wa WHO asilimia 30 ya vifo vinavyotokea nchini husababishwa na maradhi haya.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza (Tancda), Profesa Andrew Swai anasema unapokula vyakula vyenye sukari nyingi, vikiingia tumboni hukutana na hewa kisha kutengeneza nguvu ambayo huchoma baadhi ya viungo mwilini.

Kwa bahati nzuri, anasema magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuzuiwa kwa kuwa husababishwa na mtindo wa maisha lakini binadamu anahitaji chakula ili apate nguvu.

“Hilo ni zoezi la tangu kuzaliwa hivyo lazima sukari ipatikane mwilini ili ubongo, maini, figo, mapafu yaafanye kazi lakini anaonya kwamba vikizidi huleta madhara,” anasema.

Kwa kulitambua hilo, anatahadhalisha kwamba sukari inatakiwa kuingia mwilini kidogokidogo kadri inavyohitajika akibainisha matokeo ya kuzidi kwa kiasi cha sukari na moto unaotumika kuandaa nyama kuchoma…ukizidi nyama inaungua. Sukari nayo ikizidi inachoma mwili ndiyo maana wenye kisukari wanapofuka macho, mishipa ya fahamu, figo na mishipa ya damu.

Profesa Swai anasema mwili hauna uwezo wa kuizuia sukari ambayo ikikutana na hewa lazima itengeneze nguvu. “Ukianza kula vyakula vyenye sukari nyingi tangu utotoni, ukifika miaka 40 ile nguvu ya ziada iliyozalishwa na sukari inaanza kuchoma viungo vya mwili hivyo unapata kisukari.”

Kupunguza uwezekano wa kujiweka kwenye hali hii, anashauri matunda yaliwe zaidi badala ya kusagwa au kukamuliwa kupata juisi.

“Vyakula vya wanga vinaingia mwilini na vina sukari, vikifika tumboni humeng’enywa na mfumo maalumu, lakini sisi tunakosea tunapokoboa. Maganda yanakusaidia kupata choo, tukikoboa sana vinarudi mwilini na ndiyo sababu ya saratani,” anasema.

Unene kupita kiasi

Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige anasema kuna baadhi ya viashiria katika mwili endapo utajichunguza na kuvibaini, basi tambua ni mnene kupita kiasi.

Kujua kama una dalili za unene uliopitiliza, anasema mwanaume mwenye tumbo lenye zaidi ya inchi 40 likipimwa kupitia kitovuni kuzunguka kiunoni, ana kitambi na mwanamke mwenye zaidi ya inchi 35 vilevile.

“Sasa kwa mwenye tatizo kama hilo ajue kabisa ana athari ambazo zitaleta saratani, shinikizo la damu, kisukari au tatizo kati ya magoti na kitovu,” anasema.

Hata hivyo, daktari huyu anasema watu wengi bado hawajui namna sahihi ya kupunguza uzito. Anashauri kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta kwa wingi kwani hayatakiwi kuzidi asilimia 10 ili mwili ufanye kazi vizuri.

Ingawa ipo dhana kwamba magonjwa yasiyoambukiza huathiri zaidi watu wa mjini kuliko vijijini, ukweli ni tofauti.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Elisha Osati anasema tofauti iliyopo ni wakazi wa vijijini wanashiriki shughuli nyingi za kutumia nguvu kuliko wa mjini.

Lakini utafiti mbalimbali unaeleza maradhi yasiyoambukiza yanaongezeka na kuathiri hata vijijini. “Ufumbuzi wa maradhi haya si suala linalopaswa kutatuliwa hospitalini, tunatakiwa kumfikia kila mmoja kuanzia kwa wahudumu wa afya hadi kwa wananchi na hospitali iwe ni upimaji,” anasema Dk Osati.

Utafiti uliofanywa nchini mwaka 2012 ulibaini Watanzania wengi wapo kwenye hatari ya kupata maradhi yasiyoambukiza kwa viwango tofauti. Kwa wanene kupita kiasi ni asilimia ni 34.4, wanywaji pombe asilimia 29.3, wenye lehemu nyingi mwilini ni silimia 26 na wanaotumia tumbaku asilimia 15.

Hali ikiwa hivyo, gharama za matibabu zinazidi kupanda kila siku. Kwa mujibu wa utafiti wa jarida la afya la Lancet, ifikapo mwaka 2030 gharama za matibabu ya kisukari zitaongezeka hadi Dola 16.2 bilioni za Marekani (takriban Sh40 trilioni) kwa nchi za Tanzania, Kenya na Ethiopia likiwa ni ongezeko la Dola 3.8 bilioni ikilinganishwa na mwaka 2015.

Kwa miaka kadhaa, Serikali imewekeza kwenye matibabu ya maradhi ya moyo nje kwa kuwafundisha wataalamu wa ndani na kununua vifaatiba na dawa ili kupunguza idadi ya wanaofuata huduma hizo nje ya nchi.

Katika juhudi hizo, imejenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo takwimu zake zinaonyesha Watanzania wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa matatizo ya moyo imepungua tangu Julai 2017.

Mwaka 2012 wagonjwa 159 walienda kutibiwa nje ya nchi lakini mwaka 2016 walikuwa wanne tu.

Rais mstaafu wa MAT, Dk Obadia Nyongole anasema wenye maradhi ya moyo wanatumia gharama kubwa katika matibabu. “Ni lazima tujikite zaidi katika kuzuia, kuliko kutibu,” anashauri.

Kwa sasa, wagonjwa wa saratani wanaotibiwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) imeongezeka kutoka 22,000 mwaka 2017 hadi kufikia zaidi ya 30,000 mwaka jana.

Mkurugenzi wa kinga ya saratani ORCI, Dk Crispin Kahesa anasema kwa miaka mitatu iliyopita, wagonjwa wapya waliohudumiwa wameongezeka kutok 4,500 hadi 7,300.

“Hii inatuambia kuna ongezeko la wagonjwa wa saratani. Takwimu za nyuma asilimia 10 ya wagonjwa wa saratani walikuwa wanaweza kufika hospitalini lakini kwa sasa ni zaidi ya asilimia 30. Wengine hawafiki kwa kutegemea tiba mbadala ingawa wapo wenye imani za kidini,” anasema.

Taarifa ya Septemba 2018 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utafiti wa Saratani (AIRC) inaonyesha kuwapo kwa wagonjwa wapya 42,060 huku 28,610 wakifariki dunia kila mwaka nchini.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Yunus Mgaya anasema ni vyema Serikali ikatenga bajeti kupambana na maradhi yasiyoambukiza.

“Katika utafiti ambao huwa tunaofanya tunaangalia namna ya kupunguza au kutokomeza kabisa maradhi yasiyoambukiza kwa kuzingatia viashiria vinavyosababisha,” anasema Profesa Mgaya.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema Serikali imetunga sera dhidi ya magonjwa hayo lakini changamoto iliyopo ni namna ya kuwahamasisha wananchi wengi zaidi.

Wakati Waziri Mwalimu akisema hayo, nchi imebakiza mwaka mmoja tu wa kutimiza malengo hayo (2016-2020), kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti (NCDs).

Mpango huo unatekelezwa kutokana na ongezeko la maradhi haya yanayokadiriwa kuchangia asilimia 27 ya vifo nchini.