MAONI: Nida iwezeshwe ili kuongeza ufanisi wa utendaji

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) katika siku za karibuni imekuwa ikitupiwa lawama kutoka pande nyingi kwa jinsi ambavyo imekuwa ikishughulikia suala la vitambulisho hivyo.

Kimsingi yamekuwepo malalamiko ya vitambulisho kuchelewa au wengine kufuata taratibu zote na baadaye kujikuta majina yao hayamo kwenye mfumo na hivyo kukosa vitambulisho au hata namba.

Kumekuwa na kilio kila kona ya nchi kuhusu wananchi waliopitia taratibu zote ili kupata vitambulisho lakini mpaka sasa wengi hawajapata vitambulisho vyao.

Maeneo mengi nchini kuna watu wamemaliza taratibu za kupata vitambulisho mwaka jana na hadi sasa hawajapata vitambulisho vyao.

Na hamasa ya uchukuaji vitambulisho hivyo imeongezeka kutokana na watu kutakiwa kusajili laini za simu kwa alama za vidole kwa kutumia vitambulisho vya taifa.

Mwaka jana Rais John Magufuli alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk Arnold Kihaule kwenda Morogoro kutatua changamoto mbalimbali za malalamiko ya wananchi kuhusu utoaji wa vitambulisho vya taifa.

Pia majuzi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alimtaka Dk Kihaule aende mkoani Lindi atatute matatizo ya vitambulisho vya taifa.

Lawama zimekuwa nyingi dhidi ya Nida na inaonekana Nida wameelemewa na wingi wa watu wanaohitaji vitambulisho hivyo.

Serikali kwa upande wake imefanya mabadiliko ya kiutawala na kiutendaji Nida ili kuongeza ufanisi lakini inasikitisha kwamba bado utoaji wa vitambulisho kwa wananchi umekuwa wa kusuasua katika sehemu mbalimbali nchini.

Foleni katika ofisi za Nida zimetamalaki, wananchi wanaohitaji huduma hiyo ili kuwawezesha kupata vitambulisho watakavyovitumia kwa shughuli mbalimbali ikiwamo usajili wa laini za simu.

Mahitaji ya vitambulisho yamekuwa makubwa kutokana na muda wa usajili uliopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwa Desemba 31 lakini Rais Magufuli akaongeza muda wa kusajili hadi Januari 20 mwakani, ambapo baada ya hapo laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa zitazimwa.

Huku Januari 20 ikiwa ndio siku ya mwisho ya kusajili laini kwa mfumo wa alama za vidole, upatikanaji wa kitambulisho bado hauna kasi nzuri.

Wakati kazi ya utoaji vitambulishoi ilipoanza, ilichukua takriban wiki mbili kwa mhitaji kutumiwa ujumbe unaompa namba yake na baadaye kumjulisha kuwa kitambulisho chake kiko tayari.

Hata hivyo, pamoja na lawama zote ambazo zimekuwa zikielekezwa dhidi ya Nida lakini bado taasisi hiyo nayo inapaswa kuangaliwa kama imejitosheleza kwa nyenzo za kufanyia kazi na kifedha zaidi.

Ushauri wetu kwa Serikali tungependekeza kwa kiasi kikubwa iwezeke katika Nida katika suala zima la rasilimali watu na fedha ili kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Suala la utoaji vitambulisho si operesheni ya muda mfupi kutokana na ukweli kuwa si la suala la kumalizika leo ama kesho.

Kutokana na ukweli kwamba kila siku watu wanatimiza umri wa miaka 18, kwa hiyo Nida inahitaji vitendea kazi vya kudumu ili iweze kukidhi mahitaji ya taifa ya kitambulisho hicho.

Tukumbuke kuwa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana kwa hiyo lazima iwepo mipango ya kudumu ya kufanikisha shughuli za Nida na kuiacha kufanya kazi kwa operesheni.

Nida ikifanya kazi kwa ufanisi maana yake hatutasikia malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya adha wanazopata katika kufukuzia vitambulisho hivyo.