UCHAMBUZI: Q Chillah afahamu malalamiko hayamtatulii matatizo yake

Waswahili hunena yakuwa “Juzi na jana si kama ya leo.” Semi hiii na nyingine nyingi toka kwa Waswahili hunipa hekima na tafakari pana katika maisha ya jana, leo na kesho.

Katika uhalisi wenye uhalisia juzi (Mwanzo) ya wanamuziki wa kizazi kipya ni katika ugumu mkubwa katika ufanyaji wake, na hii ni katika kupata nafasi ya kurekodi tu achilia mbali swala zima la kuweza kupata nafasi ya wimbo kusikika katika vituo vya Radio.

Jana (Katikati) ya muziki huu wa kizazi kipya ni katika upana wa kusikika vyema kwenye vyombo vya habari huku mashabiki wakiongeza kwa ukubwa na kuweza kushiriki katika matamasha mengi ikiwa ni sehemu kuu ya burudani.

Ni wazi jana ya muziki imekuwa ni yenye upana wa mashabiki kuweza kufuatilia mno kazi za wasanii wao pendwa ambapo pia ununuzi wa kazi ulikuwa mkubwa mno na fahari ya mashabiki ni kufuatilia tu kazi ya msanii si kingine.

Leo ya muziki ni katika fursa pana ya uwingi wa mashabiki maana nguvu ya mitandao ya kijamii imeongeza vyema wasanii kuweza kutangaza kazi zao na hata kuwasiliana na mashabiki wao kwa ukubwa ukitofautisha na zamani ambapo njia ilikuwa ni vyombo vya habari pekee.

Licha ya leo kuwa na wepesi juu msanii kutangaza kazi yake au bidhaa, lakini imekuwa changamoto kubwa kama tu asipokuwa makini katika kuzungumza juu ya wimbo katika nyakati apatazo mahojiano ya kutambulisha.

Maana usikivu wa walio wengi ni katika matendo si kazi kama juzi na jana ya muziki huu. Hivyo wenye kujua vyema namna ya kuzungumza bidhaa zao ndiyo wenye kufanikiwa kila leo.

Mwanamuziki Darassa ni mfano halisi wa namna ya kuzungumzia bidhaa yake katika nyakati kamili. Ikumbukwe Darassa alikuwa kimya takribani mwaka mmoja lakini alivyorudi rasmi 2019 alijitahidi kukaa katika nafasi yake.

Ni kwa nini ameweza kuwa katika nafasi yake? Ni wazi alipopata mahojiano alizungumza kwa upana juu ya wimbo au bidhaa yake aliyonayo mkononi nyakati hizo.

Alitumia nguvu kubwa katika kuaminisha mashabiki kuwa wimbo wake wa nyakati hizi ni bora. Na hii ni maana halisi ya mahojiano katika kutangaza wimbo kwa msanii.

Darassa hakutumia muda aliopewa katika kueleza historia ya kuwa kimya kwa mwaka mzima, maana hata angeeleza kwa upana haiwezi kusaidia katika mwendo wa kusonga mbele katika muziki wake.

Changamoto ni kwa kaka yangu Q Chillah ambaye mchango wake katika sanaa wala si wa kuuliza. Kazi alizowahi kufanya na kutamba nazo zinamfanya kuwa miongoni mwa wasanii walioufikisha hapa muziki wa Bongo Fleva.

Kwa kifupi huwezi kutaja mafanikio ya Bongo Fleva bila kuhusisha jina lake katika orodha ya wasanii waliopigana kufa na kupona.

Lakini sasa hali ni tofauti kidogo. Q Chillah zamani akiitwa Q Chief ameshindwa kujua yakuwa malalamiko hayatatui tatizo bali maamuzi.

Kutwa kucha atoapo wimbo na apatapo mahojiano yeye ni mwenye malalamiko tu ya kubaniwa. Na Siachi kujiuliza anabaniwa na nani? Na kwa nini abaniwe? Na huyo ambaniae anapata nini?

Lakini je, anabaniwa kituo gani? Mbona vingine vinampa mahojiano? Kwa nini muda ambao anapewa mahojiano katika vituo vingine asizungumzie kwa mapana na ukubwa juu ya wimbo wake? Kwa nini atumie katika malalamiko?

Muda ambao hutumia msanii Q Chillah kutoa malalamiko ungekuwa ni mzuri zaidi wa yeye katika kupambana na kusifu kazi yake hakika angefanikiwa kwa hali ya ukubwa.

Nionavyo mimi Q Chillah anajiangusha mwenyewe kwa kinywa chake wala si watu kama adhaniavyo maana kinywa chake kimejaa kueleza malalamiko na si kueleza kazi yake katika nyakati kamili.

Uhalisi ni katika wimbo wake wa Tikisa ambao ametoa Aprili mwaka huu 2019, ni wimbo mzuri wenye usasa tupendao wengi lakini nguvu ya malalamiko imekua kubwa kuliko kuzungumzia wimbo na kuutangaza.

Vivyo chanzo cha kupotea kwa wimbo wake wa Tikisa ni yeye mwenyewe, ingawaje ni mzuri na wenye ubora.

Kesho ya Q Chillah ya kuweza kufanya vyema kwenye muziki bado ipo kwa ukubwa kama tu ataamua kuzungumza juu ya kazi zake si kuzungumza katika malalamiko ambayo hayana faida ya maana katika mwendelezo wake.

Nimalize kwa kusema Dunia ni Mapambano. Kila mtu anapambana kufaidika na jasho lake sasa usitegemee mtu atoe kukunufaisha wewe.

Jukumu la kufanya vizuri kwa Q Chillah analo mwenyewe. Atoe kazi nzuri, atoe kwa wakati naamini hakuna kituo kitakachoacha kucheza kazi nzuri.

Mwandishi ni mchambuzi wa makala za burudani.
Anapatikana kwa simu O719476068
Email: [email protected]
Instagram @iambatro Twitter @iambatro