UCHAMBUZI: Serikali ije na mkakati kusaidia wavuvi wadogo

Muktasari:

  • Zuio hilo lilitangazwa Januari, mwaka huu na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina baada ya zana nyingi zilizokuwa zikiingizwa nchini kuwa haramu ambazo zinasababisha kuvuliwa kwa samaki walio chini ya kiwango kilichopendekezwa.

Serikali imetoa kibali cha kuanza kuingiza nchini zana za kuvulia samaki ikiwa ni miezi minane tangu ilipozuia kuingizwa zana hizo kutoka nje ya nchi.

Zuio hilo lilitangazwa Januari, mwaka huu na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina baada ya zana nyingi zilizokuwa zikiingizwa nchini kuwa haramu ambazo zinasababisha kuvuliwa kwa samaki walio chini ya kiwango kilichopendekezwa.

Vilevile Serikali imetoa fursa kwa viwanda vya ndani kuzalisha nyavu zenye ubora unaokidhi mahitaji kwa ajili ya kuvulia samaki.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, wavu wowote halali unatakiwa kuwa na wima wa macho 26 tu.

Macho hayo (matundu) yanatakiwa kuwa na urefu wa inchi sita lakini chini ya hapo, zana hiyo inakuwa haramu. Kwa upande wa nyavu za dagaa, ofisa huyo alisema jicho lake linatakiwa kuwa na milimita nane.

Kutokana na sheria hiyo viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Uvuvi na Mifugo wamekuwa wakiwakamata wavuvi walio na zana zisizokidhi vigezo hivyo na kuwatoza faini, na tumeshuhudia tani kadhaa za zana haramu zikiteketezwa kwa moto.

Miongoni mwa zana zilizokuwa zinakamatwa na kuteketezwa ni pamoja na nyavu za dagaa; ndoano za sato; makokoro; timba; tupatupa; migono na timba.

Kamatakamata hiyo ya zana haramu ilisababisha robo ya wavuvi waliosajiliwa kuvua katika mialo 641 ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kurudi mitaani kuendelea na shughuli zingine baada ya zana zao kukamatwa na kuteketezwa moto.

Juzi akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Mwanza akitembelea viwanda vya uzalishaji wa samaki, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema zana ambazo zimeruhusiwa kuingizwa nchini hadi sasa ni makontena matatu ya nyavu za dagaa na kontena moja la makila, zana ambazo ziikuwa zimezuiliwa katika mpaka wa Sirari tangu Januari.

Ulega aliwahakikishia wakazi Tarime mkoani Mara na Ukerewe, Mwanza kuwa ametoa kibali cha kuingiza zana hizo na kwamba siku chache zijazo bidhaa hizo zitakuwa za kutosha sokoni.

Hata hivyo alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kulinda viwanda vya ndani na kuongeza ajira pamoja na kuepusha hasara wanazopata wavuvi huku akishauri viwanda vya ndani kuona suala hilo kama funzo kwao.

Pamoja na Serikali kutoa kibali cha kuingiza zana hizo ambazo zitauzwa kwa gharama nafuu, ni vyema ikatengeneza mazingira mazuri ya wavuvi ikiwa ni pamoja na kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili waweze kujiajiri.

Ikumbukwe kuwa kupitia operesheni Sangara iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka huu, mamia ya wavuvi walikamatwa na kutozwa faini huku zana zao zikiteketezwa.

Ni kweli Serikali ilikuwa na nia nzuri ya kulinda rasilimali za Ziwa Viktoria, lakini imesababisha maumivu kwa baadhi ya wavuvi hususan wale wadogo ambao huenda walinunua nyavu hizo kwa kujua au kutokujua.

Hivyo, niiombe Serikali iliangalie suala la kuwapatia mikopo vijana hao ambao wengi walirudi mitaani ili wapate mitaji ya kuanzia kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Pia, agizo la Ulega lisaidie wazalishaji wa nyavu hizo kutoka viwanda vya ndani kuzingatia mwongozo wa kutengeneza zana bora na zenye gharama nafuu ili kuondoa uagizaji wa zana hizo nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Vilevile ukamataji wa zana haramu unaoendelea katika mialo mbalimbali nchini iwe fundisho kwa wavuvi wengi na wazingatie sheria na taratibu za uvuvi ili kuepuka msuguano usio wa lazima.

Niiombe Serikali ije na mpango mkakati wa kudhibiti mipaka isiyo rasmi ambayo inatumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kuingiza zana haramu za uvuvi.

Natambua kuwa Serikali imeanza kutekeleza baadhi ya ahadi ikiwemo ya ununuzi wa boti za kukabiliana na wavuvi haramu, hilo bila shaka litasaidia kupunguza matukio ya uvuvi haramu.

Kwa mfano, Wilaya ya Ukerewe mwaka 2017/18 ilikamata zana haramu 96,016 zenye thamani ya Sh1.9 bilioni.

Halikadhalika tani 5,227 za samaki waliovuliwa kinyume na sheria zenye thamani ya Sh20.9 milioni zilikamatwa na watuhumiwa sita kutiwa mbaroni.

Hiyo ni wilaya moja tu bila shaka juhudi zaidi zikiendelea, mapambano hayo yanaweza kuzaa matunda, lakini wavuvi nao ni vyema wakakumbukwa.

0757708277