Serikali ilipatie ufumbuzi suala la wavuvi

Muktasari:

  • Hata hivyo, Serikali iliingilia kati na kutoa msimamo wake kupitia kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyeviagiza viwanda hivyo kuendelea kununua samaki kwa bei ya awali ambayo ni juu ya Sh8,000 badala ya Sh4,500 waliyokuwa wanataka kununulia.

Oktoba, 2018 Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu) kilitangaza mgomo wa muda usiojulikana na kusitisha kupeleka samaki kwenye viwanda vya kuchakata samaki aina ya sangara kwa kuwa vilitaka kununua kwa Sh4,500 kutoka bei ya awali ambayo ilikuwa Sh7,800 kwa kilo moja.

Hata hivyo, Serikali iliingilia kati na kutoa msimamo wake kupitia kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina aliyeviagiza viwanda hivyo kuendelea kununua samaki kwa bei ya awali ambayo ni juu ya Sh8,000 badala ya Sh4,500 waliyokuwa wanataka kununulia.

Baada ya mvutano wa bei ya samaki kati ya wavuvi na wamiliki wa viwanda, Serikali ilitoa bei elekezi ya Sh5,500 kwa kilo moja.

Pamoja na bei hiyo elekezi kutoka bado ni changamoto kwa wavuvi hasa ukizingatia gharama kubwa ya uendeshaji na upatikanaji wa vifaa vya uvuvi kuwa ghali zaidi

Kwa mfano, mafuta ya petroli lita moja sasa inakaribia Sh2,500 wakati kipindi cha nyuma yalikuwa Sh2,100; nyavu Sh 17,000 kutoka 40,000 kwa moja wakati boya katoni moja ni Sh350,000 kutoka bei ya awali ya Sh160,000 na kwa upande wa kamba ikifika Sh240,000 kutoka 190,000.

Katibu wa Tafu, Jephta Machandalo anasema bei wanayouzia viwanda vya kuchakatia samaki ni tatizo na anaiomba Serikali kuiangalia upya, lakini pia ikubali wavuvi wavue samaki wenye urefu wa sentimita 85 na kuendelea.

Kwa mujibu wa katibu huyo, Ziwa Victoria linatumiwa na nchi tatu kwenye shuguli za uvuvi huku Tanzania ikitumia asilimia 51, Kenya sita na Uganda 43.

Anasema wavuvi wa nchi za Kenya na Uganda hufaidika zaidi na shughuli hizo kuliko wale wa Tanzania kwa kuwa wanaruhusiwa kuvua samaki wa sentimita 50 na kuendelea, lakini kwa nchini jambo hilo limekuwa ni haramu, hivyo kufanya soko kuwa gumu.

Katibu huyo anasema licha ya nchi hizo kuruhusu wavuvi wake kuvua samaki wa kubwa huo, pia nchi zote tatu zinatumia nyavu nchi za sita ambazo ukubwa unatofautiana ambapo kwa Tanzania wanatumia kipande kimoja cha nyavu ngazi moja chenye matundu 26 huku Uganda na Kenya wakitumia vipande vitatu yaani ngazi tatu zenye matundu 78.

Hata hivyo, Sheria ya Uvuvi namba 22 ya 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 kifungu cha 90 (1), inataka samaki wanaovuliwa waandaliwe katika mazingira yanayokidhi vigezo vya usalama kwa mlaji na kwamba ni kosa kisheria kuvua au kuchakata sangara walio chini ya sentimeta 50 kwa kuwa ni wachanga na sentimita 25 kwa upande wa sato.

Pia, sentimita 85 kwa sangara kwa kuwa ni wazazi wanaotakiwa kundelea kuzaa, lakini sheria hiyo haiwabani wavuvi wa nchi jirani.

Kutokana na hali hiyo kumekuwapo na changamoto kwa wavuvi wa kisiwa cha Igabilo na Koziba vinavyopatikana Muleba pamoja na Lukoba kinachopatikana Musoma, kunyanganywa samaki hasa wakubwa na wavuvi wa nchi hizo kwa kuwa ni haramu nchini, hivyo kuwarudisha nyuma kimaendeleo.

Mwanzoni mwa mwaka 2018, Mpina alikamata marobota 1,152 ya aina mbalimbali za nyavu zisizoruhusiwa kisheria kutumika kuvulia samaki zenye thamani ya Sh894 milioni katika msako uliofanywa jijini Mwanza na Singida, ambapo baadhi ya nyavu zilitaifishwa na nyingine kuteketezwa huku wamiliki wakitakiwa kulipa faini ya Sh120 milioni ndani ya saa 24 kwa makosa ya kufanya biashara kinyume cha sheria.

Mwaka huohuo, katibu mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi, Yohana Budeba alitaifisha na kuteketeza zaidi ya tani 200 za shehena ya nyavu haramu za uvuvi zenye thamani ya Sh2.6 bilioni zilizokamatwa katika maghala mbalimbali jijini Mwanza na kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Mpina kwenye operesheni maalumu iliyojulikana kama ‘Operesheni Sangara’.

Ni wazi kuwa Serikali inajitahidi kupambana na uvuvi haramu, lakini isiishie tu kupambana nao pekee, bali iangalie changamoto wanazokumbana nazo ili kuzitatua kwa kuwa kufanya hivyo hata uvuvi haramu utamalizika kama siyo kwisha kabisa.

Serikali pia iangalie namna ya kusimamia soko la samaki ili kuwa na bei zenye tija kwa wavuvi angalau ziendane na gharama za uendeshaji kwa kuwa wavuvi wengi wamejiingiza kwenye biashara hiyo ya samaki kwa mitaji ya mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Ni kutokana na hali hii, gharama za uendeshaji zinapozidi kuwa kubwa inawawia ugumu kwao kurudisha fedha hizo na kuzifanya benki kuwafilisi, jambo linalowafanua kurudi nyuma kimandeleo na kushindwa kujikwamua na hali ya umaskini.

Sada Amir ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mwanza anapatikana kwa simu namba 0768-920097.