Turejee upya usafirishaji wa reli tuokoe uchumi wetu

Wednesday May 16 2018

 

Mwaka 2010 niliandika makala kuhusu umuhimu wa usafiri wa reli nchini.

Hivi sasa umuhimu wa suala hilo umeonekana na Serikali imeweka juhudi kubwa kuboresha reli na kuifanya ya kisasa ili usafiri huo uweze kusaidia kuinua uchumi wa nchi.

Kwa ufupi, nitarejea yale niliyoyagusia. Nilisema, “kwa miaka zaidi ya kumi Tanzania imezungukwa na taswira iliyokomaa ya kudhoofika kwa njia kuu za usafirishaji za reli, meli na ndege kana kwamba hazina umuhimu wowote katika ujenzi na ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa watu.

“Vituo vyote vya treni vimeota magugu. Reli imegeuka kichaka. Sababu kubwa za kudhoofika huku ni Serikali kushinikizwa na wakubwa kujitoa katika kumiliki njia kuu za usafirishaji.”

Mashirika yetu ya reli, bandari na ndege yalikufa. Huu ni msiba mkubwa kwa Taifa. Athari zake zinatugusa sote na utaziona kwa macho kila pembe ya nchi.

Tanzania inatumia magari mengi ambayo yanatugharimu pesa nyingi za mafuta, vipuri na matairi. Matokeo yake ni mfumuko wa bei kwa sababu ya gharama kubwa za usafirishaji.

Kwa mfano, wakati huo, mwaka 2010 mfuko wa sementi ulikuwa unauzwa Sh9,000 katika maduka ya rejareja jijini Dar es Salaam, lakini Mwanza ilikuwa Sh18,000. Gharama za kusafirisha tani moja ya sementi ilikuwa ni Sh150,000 ilhali kwa treni ilikuwa Sh103,663.

Hapo utaona zingebaki Sh46,337 mfukoni mwa wananchi kwa kila tani ya sementi na kiasi kingine kingi katika mchele, mahindi, sukari, chumvi na kadhalika kama tungetumia reli.

Kama nchi nzima tungesafirisha kwa kiwango cha chini kabisa tani milioni tano tu kwa treni, ungepata hesabu ya Sh46,337 zidisha kwa tani 5,000,000 utapata Sh231.7 bilioni ambazo zingebaki mfukoni mwa wananchi. Hali hii inagusa kila sehemu ya Tanzania.

Huko Muleba bei ya sementi wakati huo ilikuwa ni Sh23,000 mpaka 25,000. Kumbe behewa la sementi lingekuwa linafika Mwanza na kuwekwa kwenye meli ya mizigo hadi Kemondo bila shaka unafuu wa maisha ungekuwa mkubwa kwa mkazi wa Muleba ambaye kipato cha kinaweza kuwa kati ya Sh100,000 na Sh150,000.

Usafiri wa treni pia ni nafuu sana kwa abiria, mfano nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza daraja la tatu ilikuwa ni Sh19,000 ilihali kwa nauli ya basi ilikuwa Sh50,000. Hii ina maana kuwa Sh21,000 zingebaki mfukoni mwa kila abiria anayesafiri.

Kwa hesabu hiyo endapo watu milioni moja wangetumia treni kwa mwaka 2010 ina maana Sh21 bilioni zingebaki mfukoni mwao.

Kampuni ya reli kwa wakati huo ilikuwa na wafanyakazi 3,220 baada ya kupunguzwa kutoka 6,500. Kama shirika la reli lingesimamiwa vizuri na Serikali lingetoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa maelfu ya Watanzania.

Miongoni mwa ajira rasmi ni pamoja na wahandisi wa ujenzi na ukarabati wa treni na reli, madereva wa treni, mafundi katika karakana, wahudumu katika treni za abiria, wakata tiketi katika vituo, watunza takwimu za usafirishaji mizigo, wapakua mizigo kwenye mabehewa na hata wafanyabiashara kama akina mama lishe na baba lishe katika vituo vya treni.

Kwa mfano, kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuna vituo 68 na kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kuna vituo 85. Fikiria reli ya kwenda Mpanda na ile ya Tanga, Moshi na Arusha; ile ya Mtwara na Lindi; na Tazara kuanzia Mbeya hadi Dar es Salaam. Fikiria ajira za wasomi wetu waliosomea usimamizi wa biashara, takwimu, uhasibu na kadhalika ambao wangepata ajira katika kila kituo cha treni.

Fikiria ajira katika viwanda vitakavyokuwa vinafua chuma kwa ajili ya kutengenezea mataluma, kupasua kokoto, karakana, sementi, rangi, ufyatuaji matofali, vioo, upasuaji mbao kwa ajili ya kujenga reli mpya na vituo vipya. Reli itatoa chachu ya kukua kwa viwanda vya kufua chuma, kutengeneza vipuri na kuifanya Tanzania iingie tena katika mapinduzi ya viwanda.

Hili litasaidia kukuza ubunifu, uzoefu, utafiti na teknolojia nchini katika nyanja zote za viwanda vinavyogusa reli.

Juu ya hayo, reli ni usafiri wa uhakika wenye uwezo wa kusafirisha abira wengi zaidi ya mabasi na kwa usalama zaidi pamoja na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ajali za mabasi ambavyo vimewaacha watoto wakiwa yatima na wanawake wakiwa ni wajane.

Nini kifanyike? Serikali imiliki shirika la reli, iunde upya shirika la reli na liwe na muundo wa kujiendesha kwa faida. Serikali ijenge njia ya pili kwa reli zetu zilizopo hivi sasa ili iwe rahisi kusafirisha bidhaa na abiria kwa usalama zaidi. Ujenzi huu utanguliwe na ujenzi wa viwanda vya kufua chuma ili kuzalisha chuma cha pua ambacho hutumika katika ujenzi wa reli.