UCHAMBUZI: Mkulima, mjasiriamli jifunze ufanikiwe zaidi

Kujifunza jambo jipya au kujiendeleza katika unachokifanya ni suala ambalo halijapewa umuhimu na watu wengi nchini.

Kwa wakulima suala hili ni kama vile halipo. Wakulima wengi wameridhika na wanachokifanya miaka nenda rudi, hawataki kujifunza mambo mapya kuboresha kilimo chao.

Wakulima na wafugaji hawaoni au hawajui umuhimu wa kujifunza mambo mapya. Napenda kuwashauri wakulima na wafugaji wabadilike na kuanza kutenga muda wao kujifunza zaidi ili kujiongezea maarifa na kipato.

Kuna umuhimu mkubwa wa kutafuta maarifa mapya kwa unachokifanya kila siku, iwe ni biashara au kazi yoyote unayoifanya ikiwamo kilimo na ufugaji.

Huwezi kupiga hatua nzuri kama hutataka kujiongeza kielimu na kujifunza kwa wengine jinsi wanavyofanya au walivyopata mafanikio.

Hii itakusaidia kujifunza zaidi, na kufanyia kazi changamoto unazopitia na, katika kufanya hivyo itakusaidia kujiimarisha zaidi katika shughuli zako hivyo kukuza kipato chako.

Unaweza kuwa unafanya kilimo au ufugaji kwa muda mrefu na matokeo yakawa yaleyale kila siku lakini unapobadilika katika kile unachokifanya lazima utafanikiwa zaidi ikiwa utaongeza nguvu na kuzingatia kanuni za unachofanya

Tuchukulie mfano wewe ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa na unao wawili kwa kipindi kirefu na bei ya maziwa yako inaweza kuwa ni kubwa. Naamini ukienda mahala sahihi na kupata mafunzo utabadilika na kufanya vizuri zaidi katika biashara yako ya maziwa.

Hivyo hivyo kwa mkulima aliyezoea kuvuna kiasi kile cha mazao, akijifunza kwa wengine au akijiongeza kwa kupata maarifa zaidi atapiga hatua.

Watu wanaojiongezea maarifa kwa kutembelea sehemu za kiwango cha juu, zinazoshabihiana kikazi ama kibiashara na shughuli zao hujikuta wakifanikiwa zaidi.

Inakuwa hivyo kwa sababu watajifunza kwa kuona jinsi wenzao wanavyofanya na wao watakaporudi kwao watabadili mfumo wa utendaji wao na kuachana na mazoea waliyonayo.

Kuna njia mbalimbali za mtu kujiimarisha zaidi katika mambo anayofanya kwa mfano unaweza kuhudhuria kozi za kukujengea uwezo iwe za ndani au nje ya nchi, kumhusisha mbobezi katika eneo la shughuli zako au kuwatembelea watu wanaofanya vitu vinavyofanana na vyako.

Kuna namna nyingine nyingi pia kama vile kufanya ziara za ndani au nje husaidia kutanua na kuongeza maarifa kutokana na kuonana na watu walio katika tasnia.

Jambo jingine ni kujifunza kutoka kwao na tatu utaweza kuona kwa macho mradi ambao unafanana na wako au ambao unatarajia kuufanya. Kuona tu wengine wanavyofanya itakusaidia kubadilika na kuboresha unachofanya kwa namna tofauti na uliyokuwa unaitumia awali. Kupitia watu utakaokutana nao, wanaweza kukusaidia kukua zaidi.

Kama unahitaji kukua zaidi kwa unachokifanya basi jitahidi kutafuta mafunzo hata ya muda mfupi yanayoandaliwa na mashirika mbalimbali nchini au kwenda kutembelea miradi nje ya nchi ili kujifunza zaidi.

Kwa mfano unaweza kwenda Kenya ambayo kwa Afrika Mashariki ipo juu kwenye masuala ya ufugaji, ukiwa huko unaweza kuona wafugaji wenzako wanafanya nini tofauti na wewe uje ufanye hivyo kupata mafanikio zaidi.

Unaweza kujifunza zaidi hata kwenye eneo pana la utafutaji masoko ya bidhaa kama za kilimo na ufugaji kwa kutembelea nchi unayoilenga na kupata masoko hayo.

Kujifunza ndio kila kitu si shuleni tu kwa wanafunzi bali hata kwa mkulima au mfanyabiashara ili kuongeza kipato na kukuza uelewa.

Chukulia mfano wa karanga ambazo soko lake lipo chini nchini lakini, si ajabu ukienda nchi jirani zao hilo lina soko kubwa. Kutembea na kuonana na wanunuzi kutakufanya upanuke kiusambazaji.

Kupanuka huko si kwa kipato utakachojiongezea tu bali maarifa utakayoyapata huko. Hii itasaidia kuwanufaisha wakulima wengine wanaokuzunguka kutokana na ulichojifunza endapo utawashirikisha.

Comoro kwa mfano, ni nchi ambayo haiko mbali na Tanzania, wanahitaji sana bidhaa za kilimo. Sasa kama mkulima au mjasiriamali unatakiwa kutembelea sehemu kama hizo ili kupata masoko ya bidhaa zako.

Kuna nchi ambazo hununua kwa kiasi kikubwa mazao ya kilimo na mifugo, ni wajibu wa mkulima au mjasiriamali kuhakikisha unazikamata fursa hizi huko ziliko na kuzileta nchini ili Watanzania wafaidike nazo.

Mara nyingi, ukitembelea na kuonana na wahusika badala ya kusubiri fursa zikufuate, mafanikio yako yatafunguka haraka sana.

Sekela ni mratibu wa safari za mafunzo ya kilimo na masoko.