UCHAMBUZI: Wachezaji wa kigeni wasajiliwe kwa uwezo uwanjani

I ngawa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halijatangaza tarehe ya kuanza usajili, lakini tayari klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, zimeanza mchakato wa kuwania saini za wachezaji mbalimbali.

Klabu kongwe za Simba na Yanga ni miongoni mwa klabu zilizoingia vitani kuwania saini za nyota zinazowataka kwa msimu ujao.

Wakati Simba inaonekana kupania kusajili kikosi imara cha kushindana katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga inataka kuimarisha timu yake kwa ushiriki wa mashindano ya ndani lengo ni kutwaa ubingwa msimu ujao.

Simba imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo.

Yanga itacheza ligi ya ndani baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikifuatiwa na Azam iliyoshika nafasi ya tatu.

Simba na Yanga zimekuwa na tabia ya kusajili idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kinapofika kipindi cha usajili.

Ni jambo jema klabu kusajili wachezaji wa kigeni kwa kuwa wanaongeza ushindani wa namba kwa wachezaji wazawa.

Hata hivyo, uzoefu unaonyesha idadi kubwa ya wachezaji wanaosajiliwa tena kwa bei mbaya hawana ubora unaompa sifa ya kuitwa mchezaji wa kulipwa.

Klabu zetu zimekuwa na mfumo wa kufanya usajili kwa mazoea kinapofika kipindi cha usajili.

Simba na Yanga zinaongoza kwa kufanya usajili kwa mazoea bila kufuata ripoti ya benchi la ufundi.

Pia Simba na Yanga zimekuwa zikisajili kwa kufuata matakwa ya vigogo wa klabu hizo bila kufuata utaratibu au mapendekezo ya benchi la ufundi.

Usajili wa Simba na Yanga usiokuwa na tija kwa klabu hizo umeziingiza katika mtego wa kusajili wachezaji wa kigeni wasiokuwa na faida kwa klabu.

Klabu nyingine nazo zimeiga mfumo wa kusajili wachezaji wa kigeni ambao wamekuwa mzigo kwa timu zao.

Matokeo ya usajili mbovu kwa wachezaji wa kigeni yamewaweka ‘nyota’ hao wa kigeni katika nafasi ndogo ya kubaki kwenye klabu zao msimu ujao.

Msimu uliopita kulikuwa na zaidi ya wachezaji 30 wa kigeni waliosajiliwa, lakini ni wachache ambao walizitendea haki klabu zao.

Haitashangaza klabu nyingi msimu ujazo zikawabakiza wachezaji wachache wa kigeni baada ya kupiga panga kwa kuwa hawakuwa na mchango kwa timu husika katika ligi ya msimu uliopita.

Mazoea ya kusajili wachezaji wa kigeni yanatumika vibaya kwa baadhi ya klabu kwa sababu zinasajili ‘mapro’ wasiokuwa na uwezo ambao wanakuja kuziba nafasi za wazawa.

Tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wa kigeni wakisugua benchi licha ya kusajiliwa kwa mbwembwe na mamilioni.

Pia utamaduni wa kuwapa nafasi wachezaji wa kigeni wasiokuwa na viwango bora umekuwa chanzo cha kuzidhoofisha timu zetu wa Taifa.

Wapo baadhi ya wachezaji wa kigeni wamesajiliwa kwa shinikizo la viongozi hivyo ni vigumu kuwekwa benchi licha ya kutokuwa na uwezo mzuri hali inayowanyima fursa wazawa.

Bila shaka tumeshuhudia idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni waliokuwa mzigo kwa timu husika, hivyo ni wajibu wa klabu kuacha kuingilia masuala ya ufundi na wabaki katika nafasi za uongozi.

Makocha wapewe nafasi ya kuamua wachezaji wanaowataka kwa mujibu wa programu zao za muda mfupi, kati na mrefu ambazo zitakuwa na manufaa kwa klabu.

Hakuna sababu ya kukimbilia kusajili wachezaji wa kigeni wanaokuja kusota benchi na kuacha wazawa wenye viwango bora wakipoteza nafasi na kuua vipaji vyao.

Ni vyema viongozi wa klabu kuwaacha makocha wakafanya kazi zao za benchi la ufundi badala ya kuwaingilia kama ilivyo hivi sasa.

Naamini makocha hasa wa Simba na Yanga wakipewa nafasi ya kupendekeza majina ya wachezaji wanaowataka, naamini watatoa fursa pia kwa wachezaji wazawa kupata nafasi katika vikosi.

Simba na Yanga ambazo zinatoa idadi kubwa ya wachezaji watakaounda timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ zinatakiwa kuwajengea uwezo wachezaji wazawa katika vikosi vyao, hivyo ni vyema zikatoa kipaumbele kwa wachezaji wazawa ili kupata timu imara.

Kimsingi kwa hapa Tanzania timu bora ya Taifa inaundwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza ligi ya ndani, hivyo kitendo cha Simba na Yanga kukumbatia wachezaji wa kigeni tena wasiokuwa na sifa stahiki kinatia shaka kama tunaweza kuwa na Taifa Stars bora yenye uwezo wa kushindana kimataifa.