UCHAMBUZI: Waliouvuruga uchaguzi wa mitaa waadhibiwe

Wednesday November 13 2019Musa Juma.

Musa Juma. 

Uchaguzi wa Serikali za mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu umetawaliwa na sintofahamu.

Sintofahamu ya uchaguzi huu, imetokana na vyama vya upinzani vya Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, Chauma, UPDP na hatimaye CUF kutangaza kujitoa na kutoshiriki katika mchakato huo ambao ulianza rasmi kwa uandikishaji, kuchukua fomu na baadaye kuweka mapingamizi kwa wagombea waliokosa sifa.

Kwa mujibu wa vyama hivyo, vimejitoa kutokana na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kudaiwa kuwaondoa asilimia 90 ya wagombea wa upinzani.

Wamedai kuwa wagombea wengi hasa wa upinzani wameondolewa kwa makosa madogo ya kiufundi na wengine ni ushabiki wa kisiasa wa wasimamizi.

Kwa upande wa Chadema ilikuwa imesimamisha wagombea asilimia 85 katika vijiji 12,319 sawa na wagombea 10,471 na kwa upande wa vitongoji Chadema ilikuwa imesimamisha wagombea 50,218 sawa na asilimia 78.

Hata hivyo, wagombea asilimia chini ya nne tu ndio walipitishwa kugombea nafasi mbalimbali na katika maeneo kama majimbo ya jijini Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Kilimanjaro hali ilikuwa mbaya zaidi.

Advertisement

Kwa upande wa ACT-Wazalendo iliyokuwa imefanikiwa kusimamisha wagombea 173,573 waliopitishwa ni 6,944 sawa na asilimia nne pekee.

Hali hii pia imevikabili vyama vingine vya upinzani vikiwamo CUF, TLP na vingine ambavyo wagombea wake wameenguliwa.

Naaamini jambo hili halijatokea kwa bahati mbaya kwani mambo mengi yanyosababisha kung’olewa kwa wapinzani ni vichekesho.

Kwa mujibu wa fomu zilizokuwa zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha kuna wagombea wenye elimu ya astashahada wameondolewa kwa hoja kuwa hawajui kusoma na kuandika.

Kuna wagombea wameondolewa kwa sababu zisizo na mashiko kwa mfano kuandika majina ya vyama vyao kwa kifupi, mfano Chadema badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Wapo pia wengine walioandika ACT wakatolewa, tena mmoja ikaandikwa hicho chama hakijasajiliwa.

Aidha, kuna walimu wameondolewa kwa hoja ya kutojua kusoma na kuandika kwa kuwa tu wamegombea kupitia tiketi ya vyama vya upinzani.

Lakini pia wapo walioondolewa kwa sababu ya msingi kama kujidhamini wenyewe, kutokuwa raia au hawakujiandikisha kwenye maeneo wanayogombea.

Kwa upande wake Waziri mwenye dhamana wa Tamisemi, Seleman Jafo amefanya kazi kubwa kunusuru uchaguzi huu, lakini hajafanikiwa.

Inawezekana wengi hawamuelewi Waziri Jafo, lakini wanaomjua wanatoa ushuhuda anachosema mara nyingi ndicho anachokiamini.

Kwa jitihada zake alitembelea baadhi ya mikoa ambayo ilikuwa na malalamiko na kutoa kauli kuwa kamati za rufaa zitende haki katika kupitisha wagombea.

Waziri Jafo baada ya rufaa nyingi kupokelewa ametoa maagizo mengine kuwarejesha kugombea karibu wagombea wote ambao walioenguliwa na baadaye akaitengua.

Kwa mlolongo wa matukio inaonekana baadhi ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi walipanga kuhujumu uchaguzi na wengine walikuwa wanapokea maelekezo nje ya maelekezo sahihi ya Serikali kwani walichofanya hakika kimetia doa Serikali.

Hivyo wasimamizi hawa wa uchaguzi wataponaje kwa madudu haya.

Naamini kama kweli wasimamizi hawa wa uchaguzi hawajatumwa kuwaondoa wagombea wa upinzani kwa sababu zao binafsi lazima wawajibishwe.

Nasema wawajibishwe kwa sababu wameitia doa Serikali kwa kuonyesha inaogopa kuingia katika uchaguzi ulio huru na haki.

Wasimamizi hawa wa uchaguzi wanataka kutuaminisha kuwa CCM haiwezi tena kupambana kwa haki katika chaguzi za kidemokrasia, jambo ambalo naamini si kweli.

Wasimamizi hawa wanataka kutuaminisha kuwa wananchi hawaoni kazi nzuri zilizofanywa na Serikali na hivyo hawawezi kuwachagua wagombea wa chama tawala.

Hivyo, kwa tafsiri hizi hawa wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa watawaachaje madarakani?

Kwa mantiki hiyo ili kuondoa sintofahamu hii ni muhimu, Tamisemi itafute maridhiano na wadau wenzake wa uchaguzi ambao ni vyama vya siasa kuhakikisha vinarejea kushiriki uchaguzi huu.

Kama wanavyoshauri viongozi wa dini Tanzania ni ya Watanzania wote hivyo ni busara fursa sawa kutolewa kila mwenye nia njema kuchangia maendeleo ya nchi yake apate fursa.

Naamini bado hatujachelewa kurekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza ili Watanzania washuhudie uchaguzi wenye kufuata taratibu na sheria.

Hivyo itoshe tu kutoa hoja kuwa wote ambao walitaka kuvuruga uchaguzi huu wawajibishwe na sasa wadau wa uchaguzi wote waende katika maridhiano.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu fanikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 24.

Mussa Juma ni mwandishi gazeti Mwananchi 0754296503.