Ukikosea kuokoa unaweza kuua

Saturday May 11 2019GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

By Gaston Nundumba

Kila jambo na majira yake. Kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka, wakati wa kuvuna na wakati wa kupanda, wakati wa kutafuta na wakati wa kutumia.

Kuna makosa makubwa anayofanya binadamu kila dakika bila kujua au pengine makusudi, ambayo yanaweza kumkatiza uhai wake dakika hiyohiyo anayocheza nayo. Lakini baada ya kujikuta amenusurika, binadamu hatambui bahati hiyo na kujaribu mchezo mwingine wa hatari zaidi.

Wengi tunakumbuka tukio la dereva wa magari ya mashindano yaendayo kwa kasi kubwa (langalanga) alivyopatwa na ajali kubwa na kupoteza fahamu kwa zaidi ya miezi mitatu. Kama isingelikuwa uwezo wa kifedha na kidaktari, dereva huyu aliyejulikana kama Schumacher angezindukia kaburini.

Lakini pamoja na mkasa huo wa kuogofya, watoto na mashabiki zake walizindua mashindano makubwa zaidi ya kumuenzi bingwa wao. Wengine wanajikusuru kupanda milima mirefu ya barafu ambayo ni wachache sana hunusurika kamba inapoachia au kuteleza. Wengine wameanzisha mashindano ya kuzikana kwenye barafu kwa muda unaozidi masaa 24. Pia wapo wanaoingia kwenye misitu minene kama Amazon bila kujali nyoka wenye sumu kali waliotapakaa humo.

Hayo yote ni makusudi yanayogharimu maisha ya wengi kila siku. Lakini mbali na hayo, yapo makosa mengi yanayofanywa wakati wa kutoa huduma ya kwanza bila kujua. Watu wamekuwa wakiyafanya baada ya kusikia na kuziamini huduma hizi pasipo kuthibitisha ubora wake.

Wataalamu wamezingatia haya na kujaribu kufikisha elimu kwa umma ili kupunguza madhara. Wanashauri kwamba huduma ya kwanza ni rahisi, lakini ni lazima itolewe kwa jinsi inavyopaswa.

Majeraha hayapaswi kushughulikiwa kwa muda mrefu au mfupi sana. Wengi wamekuwa wakichemsha maji ya moto na kuyachanganya na chumvi kabla ya kulifunga jeraha kwa bandeji pindi wapatapo kukanyaga moto au kumwagikiwa na maji ya moto. Hili ni kosa kitaalamu na ipo hatari ya kulifanya jeraha kuongezeka na kukosa kukauka.

Inasisitizwa kuwa huduma ya kwanza kwenye jeraha la moto ni kuliweka kwenye maji baridi kwa wastani wa dakika kumi hivi. Madhara ya moto hupenya ndani ya ngozi na kuhatarisha tishu za mwili na mishipa midogo. Huduma ya maji baridi inasemwa kuwa bora katika kuzuia zoezi hili la uharibifu lisiendelee.

Jicho ni kiungo cha mwili linachotakiwa kulelewa kwa tahadhari kubwa sana. Unapojaribu kuondoa mdudu au uchafu wowote ulioigia humo bila uangalifu unaweza kusababisha mchubuko utakaopelekea madhara ya kudumu kama upofu. Hivyo kuhudumia jicho kunatakiwa umakini mkubwa.

Inashauriwa kutumia kikombe cha maji safi kabisa kisicho na mabaki ya kemikali yoyote wala chembe au vumbi. Sogeza kikombe na kukiinamia ili jicho lipate kuwa ndani ya maji, kisha geuza uelekeo wa jicho lako kwa mtindo wa kulizungusha kwa takribani dakika kumi mpaka kumi na tano. Baada ya hapo toa kikombe na utaona uchafu ukielea humo.

Mara nyingi watu wanaotokwa na damu puani wamekuwa na imani kwamba kuelekeza uso juu kunasaidia kuzuia damu isitoke. Lakini kinyume chake kufanya hivyo kunaweza kuongeza madhara kwani damu inakwenda kuganda nyuma ya koo na kusababisha uhaba wa oksijeni.

Watu wenye tatizo hili wanashauriwa kuketi katika hali ya kawaida wakitazama mbele. Wanatakiwa kuwa na kitambaa safi na laini ili kusaidia kufuta au kuipenga damu inapozidi. Mgonjwa anashairiwa kuvuta hewa kwa wingi na mfululizo kwani hewa ya oksijeni ni muhimu sana kwa wakati huu.

Kitu kingine cha kuzingatia sana ni utulivu mara baada ya ajali. Kama ni ajali ya barabarani unaonywa kutofanya maamuzi kwa pupa. Ingawaje ni vigumu, lakini ni muhimu kutulia katika dakika tano za mwanzo. Wakati mwingine mshipa wa damu unaweza kukatika na kusubiri wewe mwenyewe usababishe msukumo ili damu iruke.

Katika kipindi hiki kutokwa na damu nyingi ni hatari zaidi kwani unaweza kupoteza fahamu na kukielekea kifo. Lakini utulivu unaweza kusaidia mgando wa damu (blood clotting) utakaopunguza upungufu wa damu. Kisha piga au mwombe mtu akusaidie kupiga namba ya dharura kutafuta msaada.

Usiache kwenda Hospitali ati kwa sababu hujusikii maumivu. Uzoefu unaonesha kuwa mtu anaweza kutohisi maumivu kwa dakika kumi mpaka masaa mawili baada ya ajali. Hii inaweza kusababishwa na mkandamizo wa mishipa ya fahamu na mshtuko wa ubongo.

Wengine hukimbilia kujificha mara wanapopatwa na ajali ya kushambuliwa na nyoka au nyuki. Hii ni hatari kwa sababu sumu ya wadudu hawa yaweza ikakupoteza fahamu na kuhatarisha maisha yako. Unashauriwa kutokeza sehemu ya wazi na kuomba msaada.

Kama upo peke yako wakati wa shambulizi la nyoka, tumia kamba au kipande cha nguo kufunga juu ya jeraha kabla hujatafuta msaada zaidi. Utasaidia kuzuia sumu isipande kwa wingi mwilini. Kama ni nyuki anza kwa kulala chini na kufunika kichwa kwa shati ulilovaa. Kufanya hivi kutawazuia kudhuru macho na kwenye sehemu za masikio.

Nyuki huogopa moto na moshi. Kama wanakufukuza nawe ukaona mahala pamewashwa moto ama panafuka moshi ujue kuwa hiyo ni sehemu nzuri zaidi ya kujisalimisha.